• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
MITAMBO: Chombo faafu kwa waundaji sharubati

MITAMBO: Chombo faafu kwa waundaji sharubati

NA RICHARD MAOSI

MASHINI za kusaga vyakula vya aina tofauti na hata matunda, zimetumika kwa miaka mingi.

Hutambuliwa kwa kurahisisha kazi kwa mfano kwa watu wanaotaka kufanya chakula kuwa nyororo na kuwezesha hasa watoto kumeza kwa haraka bila kusakamwa.

Hata hivyo, kadri ujuzi na teknolojia inavyoendelea kuimarika, watu nao wanaendelea kuvumbua aina tofauti vya vyakula, vinywaji na kadhalika ambavyo vinaweza kuwa na soko huko nje.

Kuna mashini za blenda ambazo hutumika kwa kazi nyepesi hasa katika matumizi ya nyumbani. Hata hivyo, zipo zile zinazofahamika kama heavy duty commercial blender.

Kifaa hiki kinatumika kwa shughuli nzito na mara nyingi katika sehemu za kibiashara.

Kifaa hiki hutumia programu ya kompyuta ili kuboresha mchakato wa kuandaa vinywaji, hasa katika sekta ya kilimo-biashara cha matunda au mboga.

Kifaa hiki hutumika pia viwandani ambapo shughuli ya kusaga aina mbalimbali ya vyakula na utayarishaji vinywaji huhitajika.

Kifaa hiki si cha kawaida kwani kinaweza kuandaa aina mbalimbali ya menu kwa kuzingatia mahitaji ya watumiaji wa lishe husika, na upatikanaji wa matunda kwa wakati huo.

“Ni chombo ambacho kinaweza kutengeneza aina mbalimbali za vinywaji kwa kutumia stima na hivyo basi kupunguza kazi ambayo ingefanywa na watu watatu au zaidi,” anasema Millicent Obonyo mtaalam wa lishe.

Ni mtambo ambao una programu, ambapo mtumiaji anatakiwa kuweka matunda yake au mboga kisha akaondoka, wala hana wasiwasi kwa sababu atakuwa amewekeza kwenye mtambo wa hali ya juu, na kupunguza hasara baina ya kipindi cha kuvuna na matumizi.

Programu za kompyuta zinazotumika, huweza kushirikishwa kwa kutumia USB, kisha ukabonyeza kitufe, ukaacha kifaa hiki kufuata maagizo ili kuchapa kazi.

Anaeleza kuwa ni kifaa rahisi kutumia ingawa anashauri kwamba ni vyema watumiaji kupata elimu ya kutosha katika awamu ya kwanza.

Obonyo anasema kuwa katika maswala ya kibiashara, wakulima wengi mashinani wanaokuza aina mbalimbali ya matunda, wataepuka swala la kukadiria hasara, hususan mazao yao yanapokosa soko.

“Bila kusahau mjasiriamali anaweza kutengeneza vinywaji vya aina nyingine ambavyo ni vya kipekee,” anasema.

Obonyo anasema mkulima anaweza kutengeneza hela nzuri na ya ziada, kwa kuwa wafanyibiashara wengi wamekuwa wakitengeneza vinywaji vya kawaida tu labda kutokana na maembe, machungwa, na mapapai.

Ila utaalam wa kuchanganya matunda haya yote kwa wakati mmoja utahitaji mitambo kama hii.

Isitoshe anaongezea kuwa ni kifaa ambacho kitafanya biashara ya matunda na mboga kushamiri, ikizingatiwa kuwa kila msimu huwa na aina tofauti ya mazao.

Anasema kinyume na awali ambapo watu walikuwa wakitumia visu au panga kutengeneza vipande vya matunda au mboga imepitwa na wakati.

Anasema kitu cha kuzingatia unapotumia mtambo huu ni kufahamu kiwango cha matunda au mboga ambazo utahitaji kila siku , kwa sababu soko la matunda linaweza kuwa kubwa kuliko lile la mboga.

Kwa upande mwingine, Geoffrey Olale kutoka eneo la Kitisuru, Kaunti ya Kiambu anasema amekuwa akitumia kifaa hiki kuandaa vitu vioevu kutokana na matunda au mboga.

Anasema kuwa mtambo wenyewe hudumisha usafi, kutunza ubora, mwonekano ladha na harufu ya vinywaji.

  • Tags

You can share this post!

Vurugu zasitisha mchujo wa PAA kukiwa na madai ya mapendeleo

UJASIRIAMALI: Anavyojichumia hela kama mkulima mdogo wa maua

T L