• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
ZARAA: Nafaka mpya zatoa jibu la kudorora kwa mazao

ZARAA: Nafaka mpya zatoa jibu la kudorora kwa mazao

NA SAMMY WAWERU

HUKU Muungano wa Umoja wa Kimataifa (UN) ukijiandaa kufanya kongamano la COP27 makala ya 27 kuhusu tabianchi mwaka huu, Kenya ni kati ya mataifa yaliyoahidi mchango wake kuangazia kero ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Mchango huo unashirikisha upanzi wa miti na kudhibiti viini vya gesi ya kaboni.

Kimsingi, tabianchi imeathiri mazingira, sekta ya kilimo na ufugaji ukitatizika pakubwa.

Katika mikakati kuangazia athari hizo, wakulima wanahimizwa kukumbatia mifumo, teknolojia na mbegu zenye ustahimilivu wa hali ya juu.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro), ni kati ya wadauhusika wanaojituma na kujishughulisha kusaka suluhu ya athari zinazozingira wakulima.

Shirika hilo la kiserikali aidha limeibuka na mseto wa nafaka zinazohimili kiangazi, magonjwa na wadudu.

Ratiba ya hali ya hewa nchini inaendelea kusambaratika kinyume na ilivyokuwa awali, misimu ya mvua ikikawia.

Nzige wa jangwani na viwavijeshi, ni miongoni mwa wadudu waliojiri kutokana na tabianchi.

Kuanzia uvumbuzi wa mbegu za mtama, mahindi, maharagwe na ndegu, Kalro inazitaja kuwa za ustahimilivu wa hali ya juu.

Isitoshe, uzalishaji wake umekumbatia mfumo wa uchavushaji mtambuka (cross pollination).

Kulingana na Mirriam Mutua, mtafiti kutoka Kalro tawi la Katumani, Machakos, ni mbegu zenye hulka asilia zinazopunguzia mkulima gharama ya kununua mbegu kila msimu wa upanzi.

“Mbegu yake ni mazao baada ya mavuno, zinazoweza kupandwa misimu miwili au mitatu mfululizo,” asema afisa huyo.
Kiwango cha maharagwe, Mirriam anataja Nyota, Angaza, Metameta na Faida kama aina bora zaidi.

“Mimea inapochipuka, ina uhimili mkuu dhidi ya wadudu, magonjwa na kiangazi,” aelezea.

“Hulka za mazao kuwa mbegu misimu kadhaa, zinapunguzia wakulima gharama hasa katika maeneo kame.”

Ipo nafaka hii mpya kutoka Ethiopia, inayojulikana kama Teff ambayo kwa mujibu wa maelezo ya Mirriam inaendelea kufanyiwa majaribio katika Kaunti ya Marsabit.

Mbegu hizo mpya za Kalro zinazaa kati ya miezi miwili au mitatu, baada ya upanzi ekari moja ikitoa magunia tisa ya kilo tisini.

Uzinduzi huo, ni miongoni mwa mikakati ya serikali na wadauhusika kuafikia kilimo endelevu na cha kisasa kuangazia baa la njaa na uhaba wa chakula nchini.

Athari za tabianchi zikiendelea kutesa kilimo na ufugaji, Prof Paul Kimurto Mhadhiri na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Egerton anahimiza wakulima kukumbatia mbegu zilizoboreshwa na zenye ustahimilivu wa juu dhidi ya wadudu, magonjwa na kiangazi.

“Kitambo, mvua katika maeneo kame ilikuwa ikishuhudiwa kati ya siku 120 – 140, kwa sasa ni siku 70 – 80 kwa mwaka. Ni muhimu wakazi wanaoendeleza shughuli ya kilimo wakuze mbegu zinazochukua muda mfupi kuzalisha,” ashauri Mwanasayansi huyo.

Watafiti na Wanasayansi wanaendelea kutafiti kuvumbua mbegu zinazohimili mikumbo ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Inachukua miaka saba hadi minane kufanya utafiti, unaoshirikisha Taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis) kuidhinisha mbegu.

  • Tags

You can share this post!

BIASHARA: Gharama ya juu yazima raha ya kilimo cha maua

MITAMBO: Kifaa cha kunasa wadudu waharibifu wa matunda...

T L