• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
MITAMBO: Kifaa muhimu kwa wanaokuza matunda kupunguza hasara

MITAMBO: Kifaa muhimu kwa wanaokuza matunda kupunguza hasara

NA RICHARD MAOSI

MATUNDA kama vile mapapai, machungwa, maembe, ndizi na matufaha ni mojawapo ya mazao ambayo hukuzwa sana nchini kutokana na mahitaji yake ya kimsingi na pia kiuchumi.

Kwa wakulima wa baadhi ya matunda, wanaweza kuwazia kuyaboresha ili kujiongezea mapato na kuepuka hasara zaidi kwa kuwa kuna yale yanayoharibika haraka ikizingatiwa kuwa bei ya matunda wakati mwingine huporomoka kutokana na ushindani mkali kutoka masoko ya nje.

“Msimu ambao matunda hupatikana kwa wingi sokoni unaweza kuwa kichocheo kwa mkulima kutengeneza hela nzuri ikiwa atajifundisha teknolojia ya kuongezea mazao yake thamani,” anasema Mary Mokeira kutoka eneo la Lanet, Kaunti ya Nakuru.

Mkulima hupata hasara kutokana na wingi wa mazao sokoni, jambo ambalo humsukuma kuuza mazao yake kwa bei ya chini akihofu huenda yakaharibikia shambani.

Anasema maendeleo ya teknolojia katika kilimo yanaweza kurahisisha utengenezaji wa bidhaa kama vile juisi, mvinyo na hata jamu ya matunda.

Hata hivyo, bidhaa ambayo inaweza kutengenezwa kwa urahisi kutokana na virutubishi vya matunda ya aina mbalimbali huwa ni sharubati au juisi. Anaungama kuwa changamoto kubwa inayowakumba wajasiriamali wanaoendesha shughuli ya kuunda juisi ya matunda ni ukosefu wa mashine za kisasa.

Pili, wamekuwa wakikabiliwa na shinikizo la kudumisha usafi wa hali ya juu, ikizingatiwa kuwa wengi wao bado wanatumia mbinu za kiasili kutengeneza sharubati.

Kulingana na Mokeira ili kuepuka kero hili, mkulima anaweza kutumia mtambo wa kukamua juisi na mtambo wa kupakia kupakia juisi ili kudumisha usafi wa hali ya juu.

“Uwekezaji wenyewe utamsaidia mkulima kurahisisha kazi, pamoja na kutengeneza ubora wa bidhaa na pia wanunuzi wanaonunua kwa wingi na kisha kupakia na kuwauzia wateja wengine,” anasema.

Anasema kuwa hatua zenyewe huwa ni nyepesi almradi mkulima atakuwa amejifunza teknolojia husika , hatua na malighafi inayohitajika wakati wa kusindika matunda.

Kwa upande mwingine, mjasiriamali anaweza kuongeza ujuzi na ubunifu kwa kuchanganya na kuongeza viungo vingine katika juisi yake kama vile tangawizi na limau.

Hii ikimaanisha kuwa atakuwa ametengenezea wakulima wadogo soko la kuuza bidhaa zao.

 

Clare Nyaboke kutoka eneo la Lanet, Kaunti ya Nakuru akionyesha juisi ya miwa iliyochanganywa na tangawizi na limau. PICHA|RICHARD MAOSI

Aidha anasema badala ya mkulima kuuza bidhaa ghafi tu sokoni, juisi ni mojawapo ya bidhaa ambazo zinaweza kumletea hela nzuri hususan msimu wa kiangazi wakati ambapo matunda ni adimu sokoni.

Anasema uundaji wa juisi ya matunda umekuwa biashara muhimu humu nchini hususan miongoni mwa vijana waliohitimisha masomo yao ya juu , ambao wanalenga kujiajiri.

Mtaalam wa lishe Tony Patel, kutoka Chuo Kikuu Cha Maasai Mara Kaunti ya Narok, anasema kuwa uundaji juisi ya matunda kama ya miwa, una faida nyingi katika mwili wa binadamu kutokana na sukari yake pamoja na madini halisi ya calcium, phosphorus na potassium.

Anasema kuwa biashara ya juisi ya matunda ni mojawapo ya biashara nzuri ambayo kwa kawaida huanza kwa mtaji mdogo , lakini itakuletea faida kubwa kama mjasiriamali kutokana na soko lake.

  • Tags

You can share this post!

UTAFITI: Chuo chatafiti mitishamba kutathmini ufaafu wake

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Japan wazamisha chombo cha...

T L