• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
UTAFITI: Chuo chatafiti mitishamba kutathmini ufaafu wake

UTAFITI: Chuo chatafiti mitishamba kutathmini ufaafu wake

NA LABAAN SHABAAN

NI kawaida kuwakuta wachuuzi wa dawa za mitishamba barabarani wakipigia debe bidhaa zao kuwa dawa mjarabu za magonjwa sugu na kinga ya maradhi mbalimbali.

Ila ni ngumu kuamini kama dawa hizo zimepitia mchakato wa kutathmini ubora kwa afya.

Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) kimeanzisha kituo cha kutafiti tiba kutoka kwa mimea na kuongeza thamani kwenye mazao. Kwa kimombo kituo hiki kinafahamika kama – The National Phytotherapeutic Research Centre (NPRC).

“Tunajua kuna watu wanatumia mimea kama tiba ila hatuwezi kujua kama ni mbaya ama nzuri. Tunataka kutumia kituo hiki kushawishi wanaotumia mitishamba kuleta bidhaa zao kwa uchunguzi kuthibitisha ubora ili kuimarisha afya ya jamii,” anaeleza Makamu Chansela wa KU, Profesa Paul Wainaina.

Miongoni mwa bidhaa zinazotengenezwa kiukamilifu ni mafuta ya mimea na lishe ya mifugo kutoka kwa mkalatusi, karanga, alizeti, rosemary, mahindi, mbegu za chia, kanola na mimea mingine. Baada ya kukamuliwa kutoa mafuta, mabaki hutumiwa kuwa chakula cha mifugo.

Mkuu wa kitengo hicho cha NPRC, Diana Chebet, anadokeza kuwa kitengo chake kina mashine zinazoweza kuchakata hadi tani nne za mazao kwa siku.

“Kwa sababu ya uwepo wa mashine mbalimbali za uchakataji, chuo hiki kinaweza kuzalisha bidhaa ili kupata mtaji wa kujiendeleza,” Chebet anaarifu.

Kulingana na afisa wa Utafiti na Uvumbuzi chuoni humo, Profesa Vincent Onywera, malengo ya kitengo hicho yanaenda sambamba na Ruwaza ya Kenya ya 2030 ya kustawisha maisha ya Wakenya kupitia utafiti.

“Huu ni mpango wa maendeleo ambao unatumia utafiti na tunaamini utawezesha KU kujisimamia kwa uendelevu kupitia ujasiriamali,” Prof Onywera anasema.

KU ilipata ruzuku ya miundombinu Juni 2019 kuanza NPRC kutoka kwa Hazina ya Kitaifa ya Utafiti (NRF) baada ya pendekezo la watafiti wa chuo kuidhinishwa na kisha kituo kikazinduliwa Juni 2022.

Mtaalamu wa maabara NPRC Martin Kinyanjui, anaambia Akilimali kuwa wakulima wanatakiwa kushirikiana na kituo hiki katika kusindika mazao yao ili kuongeza thamani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi mwasisi wa NPRC, Profesa Nicholas Gikonyo, kituo hiki kimevutia watafiti wa pembe zote za dunia wanaosaka tiba kutoka kwa mimea kuganga magonjwa kama vile kisukari na saratani.

Prof Gikonyo anadokeza kuwa NPRC imefikia asilimia 95 kwa utendakazi na ina ndoto ya kuwa kituo bora barani kwa utafiti wa tiba ya mitishamba.

“Tunalenga kuwa kituo cha usanifishaji cha Wizara ya Afya idara ya tiba ya kiasili. Tunaamini tutakuwa miongoni mwa wazalishaji bora wa bidhaa za mitishamba eneo hili,” Prof Gikonyo anaeleza.

Kila kitengo cha idara hii kinafanya kazi mahususi na wataalamu waliobobea ili kuwezesha ufikiaji wa ubora unaohitajika kwa bidhaa. Pia kuna idara ya kutathmini ubora wa bidhaa iliyopitia mchakato mzima wa uzalishaji.

Mtaalamu wa uchunguzi wa kibayolojia kituoni NPRC, Catherine Muthoni anasema ni muhimu mimea kuchunguzwa ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa hazidhuru watumiaji.

“Mashine tulizopokea kufanyia kazi kwenye maabara zimesaidia udhibiti wa haraka wa ubora wa viungo tunavyochunguza kutengeneza tiba na kuongeza thamani kwenye mazao,” Muthoni anaeleza.

Mafuta yanayozalishwa kutoka kwa mimea kwa mfano ubani hutumika kama dawa ya kuuwa bakteria na kuvu mbali na kuwa manukato. Bidhaa zaidi ni kama vile unga wa uji, lemon grass tea miongoni mwa nyingine.

Katika kipindi ambacho vyuo vikuu vinakumbwa na hali ngumu ya kiuchumi, miradi kama hii itasaidia taasisi za elimu ya juu kujikimu.

You can share this post!

Nassir aongea kuhusu uhusiano wake na Ruto

MITAMBO: Kifaa muhimu kwa wanaokuza matunda kupunguza hasara

T L