• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
MITAMBO: ‘Mixer’ ya kuchanganya viungo kutoka kwa matunda, kuunda keki

MITAMBO: ‘Mixer’ ya kuchanganya viungo kutoka kwa matunda, kuunda keki

NA RICHARD MAOSI

ZOEZI la kukausha matunda, mboga au nafaka ni shughuli ya jadi ambayo awali ilitumika na wanajamii kuhifadhi mazao kwa muda mrefu yasije yakaharibika, ili kuwafaa watumiaji msimu wa kiangazi.

Hata hivyo, ili kufanya shughuli yenyewe iwe nyepesi, mitambo ya kutunza na kusindika mazao ni muhimu kwa mahitaji ya kimsingi, kama vile kudumisha virutubishi asilia vya chakula.

Ndio maana katika jukwaa la kilimo-biashara, teknolojia imekuja na uvumbuzi wa kifaa cha mixer, ili kubadili taswira nzima ya sekta hii, na kuwahimiza wakulima kuendesha kilimo chenye tija.

Akilimali ilizuru eneo la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu kuangazia mtambo wa mixer machine, ambao hufanya kazi ya kuchanganya mseto wa mazao ya shambani, hususan yaliyokaushwa.

“Ni mtambo ambao unawapatia wakulima motisha ya kuendesha kilimo endelevu, wakati wakiendelea kutafuta soko, kwa bidhaa zao,” asema James Waweru ambaye ni muokaji keki , zinazotokana na matunda yaliyokaushwa.

Kulingana na Waweru ni mtambo ambao unaweza kuoka na kutengeneza keki, jamu, viungo vya lishe(spices), kutokana na matunda au nafaka.

Isitoshe kupitia taasisi ya Kenya Induastrial Research and Development Institute, wakulima wamekuwa wakipokea mafunzo namna ya kutengeneza bidhaa zinazotokana na matunda kama vile keki.

Kwa sababu hiyo Waweru alianzisha biashara yenyewe baada ya kugundua wakulima mashinani walikuwa wakiambulia hasara baada ya mazao kukosa soko.Isitoshe mazao ghafi (raw) hayakuwa yakiwapatia hela nzuri.

Aliona pana haja ya kubuni bidhaa tofauti ambazo ni mchanganyiko wa aina mbalimbali ya matunda.

Waweru hutumia mtambo wa mixer kutengeneza keki zenye fleva ya matunda kama vile matufaha, mipapai, machungwa, stroberi na tangawizi.

Aidha, hutumia nafaka kama vile shayiri, mawele, mtama na mbegu za flaxseed, kutengeneza keki ambazo huchukua sura, maumbo na ladha ya nafaka .

Anasema faida yake ni pale mkulima anapotengeneza hela nzuri, kinyume na awali wakati ambapo wakulima wengi wamekuwa wakifanya usindikaji wa aina moja tu ya tunda.

“Kutokana na mabadiliko makubwa ya teknolojia siku hizi inawezekana kutengeneza bidhaa za keki au jamu kutokana na mseto wa matunda au nafaka kwa wakati mmoja,” asema.

Aidha, aliongezea kuwa bidhaa ambazo huwa zimetengenezwa kutokana na aina nyingi ya matunda humpatia mjasiriamali kipato kizuri.

Isitoshe, Waweru anaungama kuwa mtambo wa mixer, vilevile unachukua sehemu muhimu kuwahimiza wakulima kuendesha kilimo cha aina nyingi ya matunda.

Bila kusahau kuwa kwa wakulima ambao wamejikita kwenye swala la kuongezea bidhaa zao thamani , wanaweza kutengeneza aina nyingi ya bidhaa zinazotokana na matunda kama vile keki, jamu, viungo vya lishe (spices).

Kiafya, bidhaa zenyewe zina upekee wake hususan miongoni mwa wale ambao wamekuwa wakishauriwa kula matunda kwa wingi.

Matumizi ya mtambo wa mixer.

Waweru anasema mtambo wa mixer hutumia mfumo wa mashine maalum ambazo hutumia umeme.

Kifaa hiki kina muundo wa bakuli katika sehemu ya chini ambapo nafaka au matunda yaliyokaushwa huwekwa.

Mara tu baada ya kuwasha kitufe, mixer machine huanza kuzunguka huku makapi ya nafaka yakidondolewa na kushagika.

Anasema kuwa mkulima pia anaweza kutengeneza unga unaotokana na mazao ya shambani, na kuwauzia wamiliki wa mikahawa mikubwa ama viwanda vya kutengeneza sharubati.

Isitoshe, kifaa cha mixer kina uwezo wa kuchanganya mseto wa matunda, nafaka na kutengeneza mchanganyiko maalum (uniform mixture) kulingana na recipe.

Unga huo hutumika kuoka mikate, keki na wakati mwingine kuchanganywa na kitu kiowevu kutengeneza jamu.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Vitafunio vya wimbi vyazua msisimko sokoni

UJASIRIAMALI: Ugonjwa wa lupus haujamzuia kusaka riziki...

T L