• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
UJASIRIAMALI: Ugonjwa wa lupus haujamzuia kusaka riziki kupitia ushonaji

UJASIRIAMALI: Ugonjwa wa lupus haujamzuia kusaka riziki kupitia ushonaji

NA LABAAN SHABAAN

GRACE Mwangi, 27, alifutwa kazi ya uhudumu wa duka la vifaa Juni 2021.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kufanya kazi hii kwa sababu ya hali yake ya maradhi ya Lupus: ugonjwa unaoathiri sehemu nyingi za mwili kama vile ngozi na viungo mbalimbali vya mwili.

Moja ya matatizo makubwa wanayokumbana nayo wagonjwa wa lupus ni unyanyapaa watu wakidhani pengine wamerogwa ama huenda wakawaambukiza hivyo kuishia kutengwa. Ukiugua lupus, kinga yako ya mwili hushambulia mwili wako.

Dunia ilipoadhimisha siku ya kuhamasisha jamii kuhusu lupus (Mei 10), Akilimali ilikutana na Grace akishiriki kampeni ya Lupus Awareness Walk jijini Nairobi.

Lengo lao lilikuwa kuelimisha watu kuhusu hali hii na pia kukusanya fedha kusaidia waathiriwa.

Grace, aliyesomea taaluma ya ustawishaji jamii Chuoni St Paul’s, anaamini asingekuwa anaugua lupus asingepoteza kazi aliyofanya kwa muda ili kumudu malipo ya matibabu yanayomgharimu takriban Sh30,000 kila mwezi.

“Nilifutwa kazi kupitia arafa. Bosi wangu aliniandikia ujumbe nisirudi kazini kwa sababu ya hali yangu ya afya. Nilivunjika moyo sana,” Grace anasema kwa huzuni.

“Awali mwajiri wangu aliniambia nivue vazi langu la kazi baada ya kuepukwa na kuambiwa kuwa mimi nilikuwa nafukuza wateja kwa sababu ya jinsi nilivyo,” anaongeza.

Akiwa chuoni mwaka wa 2015 alitumia wakati wake mwingi kusuka nywele, kutengeneza mapambo ya shanga na kushona mavazi kwa uzi. Aliogopa kuajiriwa kwa hofu ya kudharauliwa na kufutwa kazi kwa njia za aibu. Akaamua kurejelea uraibu wake.

“Mimi hushona mavazi mbalimbali kama njia ya kupata hela na pia kujishughulisha nisiwe na msongo wa mawazo. Wakati ninazidiwa na hali hii, hushindwa kufanya kazi kabisa licha ya kupata oda,” Grace anasema.

Miongoni mwa mavazi anayofuma ni fulana, mabegi, kofia, marinda, soksi, glavu nk. Kadhalika, hutengeneza mavazi haya kwa kurembesha zaidi kwa mitindo ya shanga mbali na kuunda bangili, mikufu na mapambo mengine.

Wateja aghalabu humpa kazi za kuunda soksi ambazo huziuza kati ya Sh350 na Sh1,000 kutegemea urefu na aina za uzi. Yakini anapokea oda hizi sana majira ya baridi.

Grace hulipisha Sh2,500 na zaidi kwa kufuma fulana na rinda. Kwa wiki hushona angalau sweta ama marinda mawili.

Binti huyu hufanya kazi hii akiwa nyumbani Kayole jijini Nairobi. Akikaa chini sana hushindwa kuinuka.

Vazi alilotengeneza Grace kutumia uzi. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kwa hivyo mara kwa mara hutumia cherahani kushona ili awe machachari kwa kufanyia viungo mazoezi. Uchovu ni moja ya matatizo mengi wanayoishi nayo waathiriwa wa lupus.

“Wateja wangu sana sana huwa mitandaoni. Mimi hupakia kazi zangu kwenye mitandao ya kijamii halafu wakiona wanapiga picha na kuniambia niwatengenezee. Wanapovaa huvutia wateja zaidi,” Grace anasema.

Mshonaji huyu ana ndoto ya kupanua biashara yake na kuboresha mitindo. Ana matumaini kuwa njia hii itamwepushia kutegemea watu kwa kujiajiri. Kupitia kujibunia ajira, Grace anaamini atafaulu kumudu matibabu ya hali yake.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: ‘Mixer’ ya kuchanganya viungo kutoka...

NJENJE: Serikali kuagiza mahindi kudhibiti bei ya unga...

T L