• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:50 AM
MIZANI YA HOJA: Juhudi anuwai zilizochangia kuvuna matokeo bora katika mitihani ya somo la Kiswahili

MIZANI YA HOJA: Juhudi anuwai zilizochangia kuvuna matokeo bora katika mitihani ya somo la Kiswahili

NA WALLAH BIN WALLAH

WASWAHILI husema kinolewacho hupata na atangaye sana na jua hujua!

Hizo ni baadhi tu ya methali zinazomhimiza mwanadamu ajitahidi bila kukata tamaa mpaka afanikiwe maishani.

Mwaka huu matokeo ya mitihani yalipotangazwa tuliambiwa habari njema kwamba watahiniwa wa darasa la nane na wa kidato cha nne walifaulu vizuri zaidi katika masomo ya Kiswahili.

Tunawapongeza pamoja na walimu wao.

Baada ya kuwapongeza, nitaje tu baadhi ya juhudi mahususi zilizochangia kuleta matokeo mazuri ya Kiswahili kwa watahiniwa wetu wa mwaka 2021!

Kwanza kabisa, mchango mkubwa ulitokana na gazeti letu teule la Taifa Leo ambalo kila Alhamisi hutenga takriban kurasa tano maalum za kutalii na kuchambua mawanda yote ya Kiswahili kuanzia Lugha na Fasihi, Mizani ya Hoja, Chakula cha Ubongo na kadhalika!

Upembuzi wa vipengele vyote hivyo hushughulikiwa kinaganaga kuwaelimisha na kuwafaidi walimu, wanafunzi na wapenzi wa Kiswahili wasomao Taifa Leo nchini na ulimwenguni kote!

Michango mingine ilitokana na juhudi za wanahabari na watangazaji wa Kiswahili fasaha kwenye idhaa za televisheni na redio zenye vipindi vilivyoteuliwa kukuza na kufunza Kiswahili kila Jumamosi asubuhi kama vile Redio Maisha, Idhaa ya Taifa KBC na nyinginezo.

Nyenzo nyingine muhimu zilizofanikisha matokeo hayo ni juhudi za walimu na wanafunzi madarasani, kuhudhuria makongamano pamoja na kuvitembelea vituo vya Kiswahili vinavyowanoa kama vile Wasta Kituo cha Kiswahili.

You can share this post!

Kamati ya Wekesa kumpokeza Raila majina matatu Alhamisi...

VALENTINE OBARA: Sonko asiwekwe pembeni, atawafaidi ODM...

T L