• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Kamati ya Wekesa kumpokeza Raila majina matatu Alhamisi achague mmoja

Kamati ya Wekesa kumpokeza Raila majina matatu Alhamisi achague mmoja

NA CHARLES WASONGA

MGOMBEA urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga atapokea majina matatu ya watu wanaopendekezwa kuhitimu ili mmoja wao awe mgombea mwenza wake.

Akiongea na wanahabari Jumatano, Mei 11, 2022 katika mkahawa wa Serena, Nairobi, mwenyekiti wa kamati iliyowahoji watu 10 kwa nafasi hiyo Dkt Noah Wekesa, alisema hawangeweza kumpa Bw Odinga majina hayo kwa sababu “ameenda Tana River kwa shughuli za kampeni.”

“Tumeorodhesha majina ya watu watatu ambao wanahitimu kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga. Hata hivyo, hatungewasilisha ripoti hiyo leo (Jumatano) kwa Bw Odinga kwani yuko ziarani Tana River. Ametuhakikishia kuwa atakuwepo kesho (Alhamisi) kupokea ripoti yetu,” akasema Dk Wekesa, ambaye ni waziri wa zamani wa Misitu.

“ Tutawasilisha ripoti yetu pamoja na alama ambazo kila mmoja wao alipata,” akaongeza mbunge huyo wa zamani wa eneobunge la Kwanza.

Bw Odinga anatarajiwa kuteua mmoja kati ya majina ya watu hao watatu waliopendekezwa na kamati hiyo ya wanachama saba.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imewapa wagombeaji wa urais na ugavana makataa ya hadi Mei 16 kuwasilisha majina ya wagombea wenza wao.

Mnamo Jumatatu, mkurugenzi mkuu wa muungano wa Azimio Raphael Tuju alisema uamuzi wa mwisho kuhusu ni nani atakuwa naibu wa Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais ni wake Bw Odinga.

Watu kumi waliojiwasilisha kuhojiwa na kamati hiyo katika mkahawa wa Serena, Nairobi ni; kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, Gavana wa Kitui Charity Ngilu, wenzake Ali Hassan Joho (Mombasa), Lee Kinyanjui (Nakuru), Wycliffe Oparanya (Kakamega), Waziri wa Kilimo Peter Munya, Mbunge Mwakilishi wa Kike Murang’a Sabina Chege, aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na aliyekuwa Mbunge wa Emgwen na Balozi wa Kenya nchini Australia Stephen Tarus.

Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi ambaye jina lake liliwasilishwa alijiondoa dakika za mwisho na kutangaza kuwa anaunga mkono Bw Musyoka.

Mahojiano hayo yaliendeshwa siku mbili; Jumatatu Mei 9 na Jumanne Mei 10.

Awali, Bw Musyoka alitisha kutofika mbele ya kamati hiyo, lakini akabadili msimamo Jumatatu usiku na kujiwasilisha. Alisema alibadili msimamo “ili wasiwe na kisingizio kwamba sikuja.”

  • Tags

You can share this post!

Shirika lazindua mpango kushirikisha vijana kutoa huduma za...

MIZANI YA HOJA: Juhudi anuwai zilizochangia kuvuna matokeo...

T L