• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 4:32 PM
VALENTINE OBARA: Sonko asiwekwe pembeni, atawafaidi ODM pakubwa

VALENTINE OBARA: Sonko asiwekwe pembeni, atawafaidi ODM pakubwa

NA VALENTINE OBARA

UAMUZI wa gavana wa zamani wa Nairobi, Bw Mike Sonko, kuwania ugavana wa Mombasa katika uchaguzi wa Agosti 9, bila shaka umeibua msisimko tele wa kisiasa Mombasa na kitaifa kwa jumla.

Mengi yamesemwa kuhusu uamuzi huo wake, kukiwa na maoni tofauti kutoka pande mbalimbali.

Idadi kubwa ya wale wanaounga mkono uamuzi wake wanasema kuwa licha ya hila zake, amewahi kuonyesha kujitolea kubadili maisha ya wananchi wa kawaida alipokuwa mbunge wa Makadara na baadaye akawa gavana wa Nairobi.

Kwa upande mwingine, wapinzani wake wanasema hafai kuwania cheo hicho kwa kuwa, kulingana nao, yeye si mkazi halisi wa Mombasa na hivyo basi hajui changamoto zinazokumba wakazi.

Mbali na hayo, wapinzani wanasema kutimuliwa mamlakani kwa kukosa maadili ya uongozi kunamfanya asiwe kielelezo bora cha uongozi Mombasa.

Hata hivyo, kwa mtazamo wa kisiasa, Sonko anaweza kuwa na manufaa makubwa kwa mgombeaji urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga.

Gavana huyo wa zamani ni mwanachama wa Wiper, ambayo inaongozwa na aliyekuwa makamu wa rais, Bw Kalonzo Musyoka.

Katika miaka iliyopita, alidhihirisha uwezo wake wa kuvutia umati mkubwa wa wananchi, si tu katika mikutano ya kisiasa bali hadi debeni wakati wa uchaguzi.

Uwezo huu wake ndio uliomsaidia kushinda chaguzi ambazo wadadisi wengi wa kisiasa hawangedhani angeshinda, ikiwemo uchaguzi mdogo wa ubunge wa Makadara ambao alishindana na vigogo wa siasa za Nairobi alipochukuliwa kuwa limbukeni.

Ijapokuwa chama cha ODM ambacho kinaongozwa na Bw Odinga kina mgombeaji wake wa ugavana Mombasa, ambaye ni mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, itabidi kutafutwe njia ya kumsitiri Sonko ndani ya kampeni za urais za Azimio Mombasa na hata Pwani kwa jumla.

Kumekuwa na ripoti kwamba baadhi ya viongozi wa ODM wanapanga kutumia sheria kumzuia Sonko asiwanie.

Ukweli ni kuwa kuwepo kwa Sonko katika kampeni za Raila kutasaidia zaidi ODM kuafikia lengo la kushinda urais kuliko kumzuia.

Kumekuwa na wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wafuasi wa ODM Pwani kwamba, kutokuwepo kwa Gavana Hassan Joho eneo hilo wakati mwingi kunaathiri kampeni za uchaguzi ujao.

Bw Joho alitegemewa sana kusimamia kampeni za Bw Odinga na wagombeaji wengine wa ODM katika chaguzi zilizopita.

Lakini kwa miezi kadhaa sasa, amekuwa akielekeza juhudi zake kwa siasa za kitaifa nje ya Pwani kwa lengo la kupanua mbawa zake.

Matarajio kuwa mwenzake wa Kilifi, Bw Amason Kingi, angalijaza pengo lake kupitia chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA) sasa yamefifia baada ya gavana huyo kujiunga na kikosi cha Naibu Rais William Ruto katika Muungano wa Kenya Kwanza.

Ikiwa kweli ODM inataka kudumisha umarufu wake Pwani ili usipunguwe ikilinganishwa na jinsi ilivyokuwa miaka iliyopita, inafaa kucheza karata zake kwa makini na kuepusha uwezekano wa kusababisha maporomoko zaidi ambayo yanaweza kuinua wapinzani wao.

Lengo la chama halifai kuwa tu kudumisha umaarufu wake bali kuuongeza, na hilo halitawezekana ikiwa hakutakuwa na mipango kabambe ya chama kuweka mipango bora ya ushirikiano na wenzake katika Azimio hata kama wanashindania nafasi nyinginezo.

  • Tags

You can share this post!

MIZANI YA HOJA: Juhudi anuwai zilizochangia kuvuna matokeo...

NGUVU ZA HOJA: Tutie bidii kuzungumza Kiswahili fasaha kama...

T L