• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
MIZANI YA HOJA: Mambo yanayokwaza maendeleo ya Kiswahili katika nchi ya Uganda

MIZANI YA HOJA: Mambo yanayokwaza maendeleo ya Kiswahili katika nchi ya Uganda

NA PROF IRIBE MWANGI

SIKU ya leo na kesho kuna warsha ya kimataifa inayoendelea kwenye mkahawa mmoja jijini Nairobi.

Warsha hii ni sehemu ya utafiti mpana unaohusu, kati ya masuala mengine, lugha ya mpito itumiwayo katika mafunzo kutoka kwenye lugha aielewayo mwanafunzi (ya kieneo/ya kwanza) hadi ile asiyoijua (Kiingereza kwa mfano).

Utafiti huu unashirikisha Chuo Kikuu cha Notre Dame, Marekani; cha Makerere, Uganda na cha Nairobi, Kenya.

Katika mkutano tangulizi wa kuratibu warsha hii, nilikutana na mtafiti kutoka Makerere aitwaye Julius Ssentongo. Nilimuuliza sababu zinazotinga maenezi ya lugha ya Kiswahili nchini Uganda na ukazuka mjadala kuhusu maenezi ya Kiswahili Afrika Mashariki.

Jambo lililojitokeza wazi ni kwamba namna Kiswahili kilivyotumiwa Uganda, na kile kilichohusishwa nacho, kilikuwa kizingiti kikuu. Hii ni kwa sababu Kiswahili kilionwa kama lugha ya ukandamizaji kwa kuwa ndiyo lugha iliyotumiwa na jeshi na polisi walipokuwa wakitekeleza ukatili wao wakati wa utawala wa kimabavu wa Iddi Amin.

Jambo jingine ambalo limetinga maenezi ya Kiswahili ni kule kuhusishwa na mtu ambaye hakupata elimu ya kutosha. Kwa wazazi wengi, iwapo mtoto hakuzungumza Kiingereza au lugha nyingine ya kigeni, hata azungumze Kiswahili mufti vipi, bado ataonekana kama ambaye hakusoma. Jambo hili pia hutatiza sana ununuzi na usomaji wa magazeti yaliyoandikwa kwa Kiswahili kama Taifa Leo nchini Kenya. Hii ni dhana potoshi.

Sitaki kutaja kwamba Kiswahili kilihusishwa na ujanja na ulaghai kwa kuwa tuliandikia hilo, lakini niseme kuwa kimetazamwa kama lugha ya vijana au ya mtaa na inayokosa ustaarabu. Haya ni baadhi ya mambo yanayotinga maenezi yake.

  • Tags

You can share this post!

Ruto ajivisha kofia aliyovaa Raila 2017

GWIJI WA WIKI: Angie Magio

T L