• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 11:39 AM
Ruto ajivisha kofia aliyovaa Raila 2017

Ruto ajivisha kofia aliyovaa Raila 2017

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amejipata katika mazingira ya kisiasa ambayo mpinzani wake mkuu katika kinyang’anyiro cha urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, Raila Odinga alikumbana nayo kuelekea uchaguzi wa 2017.

Sawa na Bw Odinga wakati huo, sasa Dkt Ruto, ambaye ametengwa na bosi wake Rais Uhuru Kenyatta, analalamikia hatua ya mawaziri kumuunga mkono Bw Odinga.

Dkt Ruto, haswa anawalaumu Waziri wa Usalama Fred Matiang’i na mwenzake wa Mawasiliano Joe Mucheru ambao wametangaza wazi kuwa wanamuunga mkono Bw Odinga.

Mawaziri wengine ambao wamekuwa wakimfanyia kampeni Bw Odinga ni Eugene Wamalwa (Ulinzi) na Peter Munya (Kilimo).

Tayari Mkuu wa kituo cha kushirikisha kampeni ya urais ya Dkt Ruto, Gavana Josphat Nanok wa Turkana, amewasilisha barua ya malalamishi kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) akilalamikia kile anachodai ni Dkt Matiang’i na Bw Mucheru kuongoza kampeni za Raila.

MATIANG’I NA MUCHERU

Wizara ya Dkt Matiang’i ndio inasimamia maafisa wa polisi watakaotoa ulinzi kwa maafisa wa IEBC wakati wa upigaji kura na kuhesabiwa.

Nayo wizara ya Bw Mucheru ndiyo inasimamia Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA) ambayo itasimamia mtandao wa 3G ambao IEBC itatumia kupeperusha matokeo ya uchaguzi.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amejibu Kenya Kwanza kuwa tume hiyo haina mamlaka ya kuwaadhibu mawaziri wanaojiingiza katika siasa za uchaguzi.

Pia kisheria mawaziri hao hawana makosa. Kulingana na sehemu ya 23 ya Sheria ya Maadili na Uongozi 2016, mawaziri katika serikali kuu na wenzao katika serikali za kaunti hawazuiwi kushiriki siasa.

Hii ni kwa sababu wao ni wateule wa kisiasa na wana wajibu wa kuendeleza sera na maongozi ya wakubwa wao.

Mnamo 2017 Bw Odinga alipolalamika kuhusu Dkt Matiang’i na Bw Mucheru kufanyia Jubilee kampeni, Dkt Ruto mnamo Julai 19, 2017 alikuwa mstari wa mbele kuwatetea mawaziri hao: “Ningependa kumwambia Raila na wenzake wa Nasa kwamba waachane na Matiang’i. Wao wanashindana na mimi pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wala sio Matiang’i na mawaziri wengine.”

Aliendelea kupuuza malalamishi ya Bw Odinga na vinara wenzake katika muungano wa NASA akidai walikuwa wamepoteza mwelekeo na hawakuwa tayari kwa uchaguzi mkuu.

MALALAMIKO YA NASA

Sawa na Bw Odinga mnamo 2017, Dkt Ruto sasa amewasilisha masuala ambayo anataka IEBC itekeleze ili kujenga imani ya Wakenya kuwa itaendesha uchaguzi huru na wa haki.

Masuala hayo ni sawa na yaliyowasilishwa kwa IEBC na muungano wa NASA chini ya unahodha wa Bw Odinga mnamo 2017.

Kati ya masuala hayo ya muungano wa Kenya Kwanza ni kutaka IEBC iweke wazi sajili sahihi ya wapiga kura katika maeneo mbalimbali ya uwakilishi.

Kwenye memoranda iliyowalishwa kwa IEBC katika ukumbi wa Bomas of Kenya mnamo Jumatatu, muungano huo pia unataka IEBC iweke wazi ripoti ya kampuni ya KPMG iliyosafisha sajili ya wapiga kura.

Aidha, kambi ya Dkt Ruto pia inataka IEBC itoe maelezo kuhusu hali ya vifaa vya kielektroniki itakavyotumia katika uchaguzi mkuu.

“Pia tunataka IEBC ieleze jinsi ambavyo maafisa wake watamudu idadi kubwa ya wapiga kura katika vituo vyote 53,000 kote nchini. Pia itoe hakikisho kuwa Serikali haitaingilia uchaguzi,” akasema Bw Nanok.

  • Tags

You can share this post!

CHAKULA CHA UBONGO: Unahitaji uchangamfu tu kuyaafiki...

MIZANI YA HOJA: Mambo yanayokwaza maendeleo ya Kiswahili...

T L