• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
GWIJI WA WIKI: Angie Magio

GWIJI WA WIKI: Angie Magio

NA CHRIS ADUNGO

ANGIE Magio alikua akitamani kuwa mwanahabari.

Wepesi wa ulimi na ufundi wa kusuka maneno ni upekee uliomfanya awe maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Alikuwa na mazoea ya kujirekodi na akapendwa na wengi – shuleni na nyumbani – kutokana na ‘sauti yake ya utangazaji’.

Hata hivyo, ndoto ya kuwa ripota na msomaji wa taarifa za habari redioni ilining’inizwa kwenye uzi mwembamba wa matumaini kabla ya kukatika ghafla baada ya babake kufariki.

Alianza kumsaidia mama mzazi katika ushonaji wa nguo huku akijishughulisha pia na masuala ya fasheni na uanamitindo.

Anakiri kuwa faraja aliyopata kutokana na kazi hizo ilimpa nguvu za kukabiliana na pandashuka za kila sampuli.

Alijiunga baadaye na kikundi cha wasakataji densi cha Shaniz Dance Troupe mnamo 2000 kabla ya kujitosa katika fani ya uigizaji akiwa mwanachama wa Kizingo Arts Troupe Mombasa.

Alitamba kwa urahisi katika majukwaa mbalimbali jijini Mombasa na Nairobi kutokana na ukubwa wa kiwango chake cha ubunifu na ufasaha wa lugha.

Alijikuza zaidi kisanaa akiwa na kikundi cha St Luke’s Arts Mombasa kabla ya kutwaliwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la Sponsored Arts For Education (S.A.F.E) Kenya kati ya 2004 na 2014.

Akiwa huko, aliongoza waigizaji wenzake kufyatua michezo kadhaa ikiwemo ‘Ni Sisi’ na ‘Watatu’ kwa lengo la kuhamasisha umma kuhusu masuala ya afya pamoja na umuhimu wa kuhifadhi mazingira, kudumisha amani na kukomesha ugaidi.

Baada ya kushiriki mchezo wa kwanza runingani akiigiza mhusika Diana katika ‘Dosari’ (KBC, 2014), milango ya heri ilijifungua na akanogesha ‘Utandu’ (Maisha Magic East – DStv, 2014), ‘Sumu La Penzi’ (Africa Magic – DStv, 2015), ‘Nishike’ (2017) na ‘The Kalimani Dynasty’ (KTN, 2019).Mbali na filamu ‘Maza’ (Maisha Magic East, 2017) iliyomtia katika orodha ya mwisho ya wawaniaji wa Kalasha Awards 2018, mchezo mwingine uliomkweza Angie hadi ngazi ya juu katika ulingo wa uigizaji ni ‘Selina’ (Maisha Magic East, 2019). Kwa sasa anaigiza mhusika Fatima katika ‘Sultana’ (Citizen TV).

Kubwa katika malengo yake kisanaa ni kuwa miongoni mwa maprodyusa wa humu nchini watakaofyatua filamu zitakazokubalika zaidi kimataifa.

Angie amejaliwa watoto wawili – Natasha Chebet na Nathan Kiptoo.

Anashikilia kuwa siri ya kufaulu katika fani ya uigizaji ni kujituma, kuvumilia, kujiheshimu na kujinyenyekeza.

Alilelewa katika mtaa wa Ganjoni, Kaunti ya Mombasa. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watatu wa Bi Anastancia Omala – mke wa kwanza wa marehemu Bw Joseph Magio ambaye mkewe wa pili, Bi Francisca Nagawa, amejaliwa watoto watatu.

Alianza safari ya elimu katika shule za msingi za Valentine na Sacred Heart zilizoko Ganjoni kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Coast Girls, Mombasa (1995-1998). Alisomea upishi na masuala ya maendeleo ya jamii katika taasisi za Marianist na East Africa Institute of Development Studies baada ya kupata ujuzi wa kiteknolojia katika Chuo cha Jara, Mombasa.

You can share this post!

MIZANI YA HOJA: Mambo yanayokwaza maendeleo ya Kiswahili...

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya Upili ya...

T L