• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
MIZANI YA HOJA: Ukitaka kufanikiwa maishani shirikiana na watu wa mawazo na malengo sawa na yako

MIZANI YA HOJA: Ukitaka kufanikiwa maishani shirikiana na watu wa mawazo na malengo sawa na yako

NA WALLAH BIN WALLAH

MAISHA ya mwanadamu ni kama maji ya mto ambayo daima yanafuata mkondo na kuteremka kwenye mabonde kuelekea baharini au ziwani.

Mabonde ndiyo yanayoruhusu na kuyasukuma maji yaongeze nguvu za kuteremka hadi baharini kwa sababu miteremko yote ya maji na mabonde huelekea upande mmoja kule kule.

Katika siri ya maisha ya mwanadamu ni hivyo hivyo kwamba watu wenye mawazo na malengo yanayofanana huelekezana vizuri zaidi. Aghalabu mawazo na maono yao hayakinzani. Ni muhali kuzozana!

Fikra zikifanana watu hufaana hata kama hawafanani kwa sura.

Ninaomba nitumie fursa hii kukurai na kukusihi wewe msomaji wa makala haya, ukiwa mwalimu, mzazi au mpenzi wa Kiswahili ama mwanafunzi kwenye likizo hapo nyumbani kwamba, uwachunguze sana watu na marafiki unaoandamana nao kila wakati.

Usishikamane na watu ambao hamwelewani. Usiwafuate watu ambao hawana tabia njema za uadilifu ambazo ungependa kuiga. Kumbuka ukiandamana na muuza uvundo utanuka uvundo. Na ukiandamana na muuza marashi utanukia marashi.

Usisahau methali isemayo kwamba nazi mbovu harabu ya nzima.Tunza sana utu wako kwa kuandamana na watu wenye tabia njema na heshima zao. Tumia akili zako vizuri kuchagua watu waungwana wa kushirikiana nao. Usije ukawa bendera kufuata upepo ama ukawa kama kumbikumbi anayefuata mwangaza wa taa hatimaye hufa motoni! Zingatia!

  • Tags

You can share this post!

Zinki na faida zake mwilini

MAPISHI KIKWETU: Supu ya kabichi tamu na chachu

T L