• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Mkenya aliyefariki katika ajali ya barabara Amerika alitarajia kuona mwanawe Februari 2024 akizaliwa

Mkenya aliyefariki katika ajali ya barabara Amerika alitarajia kuona mwanawe Februari 2024 akizaliwa

NA NYABOGA KIAGE

BW Payne Isichi Muyale, Mkenya ambaye aliaga dunia Nchini Amerika ilikuwa imesalia miezi mitano pekee mtoto wake azaliwe.

Hii ni kulingana na familia yake inayohoji mwendazake alikuwa ameenda katika nchi hiyo kusoma.

Mke wake, Bi Ashley Handley alikuwa ajifungue mwezi wa Februari 2024.

“Alihusika katika ajali na kufariki papo hapo. Aliwaacha babake, Matayo Muyale Isichi na dada zake wawili; Shimrone na Stacy. Wengine ni mke wake na mtoto ambaye bado hakuwa amezaliwa,” familia hiyo ilisema kupitia mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali.

Mke wake alisema kuwa alimpoteza mpenzi ambaye alikuwa wa maana katika maisha yake, akihuzunika itakuwa vigumu sana kumsahau.

“Ulikuwa na bado wewe ni mpenzi wangu, nitakupenda milele. Kila kukicha nitazidi kukukumbuka na kukupenda,” Bi Handley alisema.

Mwendazake aliaga dunia Julai 26, 2023 akielekea nyumbani kutoka kazini.

Alikuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Idaho State, Amerika.

Kwenye akaunti yake ya Facebook, Bw Muyale anaonekana kuwa jamaa mcheshi na aliyependa kuishi maisha raha.

Pia alionekana kuwa jamaa ambaye aliipenda familia yake sana.

“Leo ni siku ambayo tunasheherekea siku yako ya kuzaliwa. Dada yako Shimrone Slaxta anaongeza mwaka mmoja na ninafurahia kwani ameishi maisha mema sana. Kitu kimoja wengi hawajui ni kuwa, alikuwa kila wakati karibu nami,” mojawapo ya chapisho lake linaelezea.

Aliongezea kusema kuwa bila yeye, maisha yake sio mema na yeyote ambaye ni rafiki ya dadake bila shaka ana bahati sio haba.

Familia sasa inawaomba wasamaria wema kuwasaidia kusafirisha mwili wa mwendazake kutoka Amerika, kuja Kenya kwa minajili ya mazishi.

Gharama ya kuhifadhi maiti yake, imegonga kima cha Sh1.4 milioni.

  • Tags

You can share this post!

Stivo Simple Boy ajinyakulia kipusa kitu kipya, Wanja Kihii

Silvanus Osoro asema akistaafu siasa atakuwa Pasta

T L