• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 7:55 AM
Mkuzaji stadi wa matikitimaji Pwani anayetaka vijana wasilaze damu

Mkuzaji stadi wa matikitimaji Pwani anayetaka vijana wasilaze damu

Na HAWA ALI

Joseph Mrisho ni kijana anayependa sana kushughulika na masuala ya kilimo. Baada ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Mt Kenya mnamo 2019 kama mwanauchumi, hakupata ajira kwa haraka.

Aliamua kuzamia kilimo cha matikiti maji katika shamba la ekari moja, eneo la Mariakani, ambapo yeye hukuza aina ya tikitimaji ya F1 Sukari.

Mrisho anapenda kilimo hai na amekuwa akitumia muda wake kujifahamisha mengi kuhusu kilimo cha matikiti kupitia mitandao ya kijamii.

Anasimulia: “Vijana wengi tumekuwa tegemezi kwa wazazi hata baada ya elimu ya chuo kikuu. Elimu ni mtaji tosha kwa kijana, kwani, si wazazi wote wana uwezo wa kuwaendeleza watoto wao baada ya masomo. Nikiwa chuo, niliweka malengo kwamba baada ya masomo ningejishughulisha na kilimo.

“Hivyo nilijiwekea akiba ya Sh80,000 kama mtaji ili nitakapohitimu, niweze kuanza shughuli za kilimo badala ya kutafuta ajira. Niliungana na vijana wenzangu ili kuongeza nguvu zaidi, na tukafanya kilimo kwa pamoja. Nililima tikiti kwa kilimo cha umwagiliaji kiasi cha ekari moja.

“Kwa mara ya kwanza sikupata faida kwani sikuwa na uzoefu mkubwa na changamoto zilikuwa ni nyingi. Sikukata tamaa nilirudia tena mara ya pili na kupata faida, naipenda kazi hii na napenda kushirikiana na vijana wenzangu ili tufanye kwa ukubwa zaidi.’

Joseph anafichua kwamba kilimo cha matikiti maji kina soko kubwa, haswa maeneo ya pwani yenye joto jingi. Japo wanunuzi huja shambani mwake kununua kwa zamu, yeye pia husambaza katika miji ya Mombasa, Malindi na Kilifi na sehemu nyinginezo za Pwani.

“Ni matunda yasiyohitaji mtaji mkubwa zaidi lakini mazao huwa ni mengi na ya kurudhisha,” aongeza.

Kwa kawaida yeye huuza kati ya Sh80 na Sh500 kulingana na kilo za tikitimaji lenyewe. Wanaouza rejareja huuza kwa vipande vipande ambapo kimoja huuzwa kwa kati ya Sh10 na 30.

Yeye huuza mfuko mmoja wa tikiti maji la kilo mia kwa kati ya Sh3,000 na Sh4,000. Kwa msimu mmoja, yeye huunda takriban Sh300,000 na baada ya makato na gharama mbalimbali yeye husalia na Sh240,000.

Joseph anasema kwamba hajapata changamoto yoyote ya mbegu kwani zinapatikana katika maduka mbalimbali ya kilimo almaarufu Agrovets.

Changamoto kuu ni kuharibika kwa matunda hayo haswa yanaposafirishwa na wakati mwingine pia kukosa soko la kutosha.

“Kila tunda lina msimu wake, hivyo wengi hawataki kula matikiti maji kwenye msimu wa maembe,” anaongeza.

Changamoto nyingine ni kwamba baadhi ya wateja hupendelea aina Fulani ya tikiti ambayo si ile anayokuza.

“Wakati mwingine kuna wale wanaotaka Sugar Baby, nami nakuza Asali F1, wanayanunua lakini bila kutosheka. Aina ya Asali F1 hufanya vema katika udongo huu kuliko aina nyingine ya tikiti maji,” aliongezea.

Kuna aina mbalimbali za tikitimaji kama vile, Asali F1, Sugar Baby, Charleston Grey, Andaman 631 F1, Crimson Sweet na kadhalika.

Wapo wadudu hatari ambao hushambulia matunda haya na jambo hili limeathiri mapato yake kwa asilimia kubwa mno.

“Kuna mdudu anayeitwa Melon fly ambaye ni hatari zaidi na husambaa haraka sana kutokana na uwezo wake wa kuangua mabuu wengi kwa wakati mfupi. Wao hutaga mayai zaidi ya 1,000 na huyaangua takriban yote,” alisikitika.

Kutokana na hali hii, mdudu huyu mmoja wa kike anaweza kuharibu matikiti mengi sana katika uhai wake.Anakiri kwamba ameweza kufanya mengi kupitia kilimo cha matikiti maji.

Amejenga nyumba yake pamoja na kuwajengea wazazi wake nyumba na pia kujinunulia gari dogo la kubeba matikiti hayo anapoyauza katika miji mbalimbali.

Anawashauri vijana kukumbatia kilimo na kutia bidii kazini ili kujikomboa kutokana na minyororo ya umaskini

You can share this post!

AKILIMALI: Mitishamba matibabu tosha kwa ng’ombe wake

Vigezo muhimu vya kuzingatia kufanikisha kilimo cha blue...