• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
MUME KIGONGO: Kunenepa matiti ni kawaida lakini kunaweza kuwa tatizo la kiafya pia

MUME KIGONGO: Kunenepa matiti ni kawaida lakini kunaweza kuwa tatizo la kiafya pia

NA LEONARD ONYANGO

KUONGEZEKA kwa ukubwa wa matiti miongoni mwa wanaume (gynecomastia) ni tatizo la kawaida.

Watafiti wanasema kuwa karibu nusu ya wanaume kote duniani wamewahi au watapatwa na tatizo hilo katika siku za usoni.

Matiti ya vijana wa kiume hunenepa wakati wa kubaleghe kutokana na mabadiliko ya homoni mwilini na kurejelea hali ya kawaida baada ya kipindi hiki.

Karibu asilimia 60 ya watoto wa kiume huzaliwa wakiwa na matiti makubwa lakini hurejelea hali ya kawaida baada ya wiki tatu. Ukubwa huo wa matiti husababishwa na kuzaliwa na homoni nyingi zinazofahamika kama estrogen kutoka kwa mama.

Lakini madaktari wanasema kuwa kufura huko kwa matiti kunaweza kuwa chanzo cha msongo wa mawazo miongoni mwa vijana wanapochekwa na wenzao.

Tofauti na kansa ya matiti ambayo huathiri titi moja, gynecomastia hufurisha matiti yote mawili.

Kulingana na madaktari, hali hii inaweza kusababishwa na matumizi ya dawa kama vile tembe za kupunguza makali ya kansa ya korodani, virusi vya HIV, vidonda vya tumbo (ulcer) na maradhi ya moyo.

Ubugiaji wa pombe na matumizi ya mihadarati kama vile bangi na heroini, yanaweza kusababisha matiti ya wanaume kunenepa.

Lakini wataalamu wanaonya kuwa matiti yanapofura na kutoa usaha au kuhisi maumivu, unafaa kumuona daktari mara moja.

Maumivu, haswa yanapokuwa kwenye titi moja, yanaweza kuwa dalili ya kansa ya matiti.

Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa wanaume wanachangia asilimia 12 ya visa vya kansa ya matiti humu nchini.

You can share this post!

Owino: Hatuendi kutalii Ghana bali kushindana

Pigo kwa Ruto Jubilee ikifufuka Mlima Kenya

T L