• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
Mwalimu anayedaiwa kuwaua wanawe atiwa mbaroni

Mwalimu anayedaiwa kuwaua wanawe atiwa mbaroni

NA MWANGI MUIRURI

POLISI katika Kaunti ya Mombasa mnamo Desemba 27, 2023, wamemtia mbaroni James Gitau Karanja aliyekuwa mafichoni tangu Desemba 20, 2023, alipotoweka baada ya kudaiwa kuwaua kinyama watoto wake wawili katika Kaunti ya Murang’a.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Murang’a Bw Mathiu Kainga, maafisa kutoka Kaunti ya Mombasa ndio waliofichua kukamatwa kwa Bw Gitau mwenye umri wa miaka 33 na ambaye ni mwalimu wa Shule ya Upili ya Kamacharia iliyoko eneobunge la Mathioya.

“Tumearifiwa kwamba mshukiwa huyo alikamatwa katika soko la Kongowea alipokuwa katika harakati za kusaka chakula cha mchana na raia mmoja akamtambua kutokana na picha zilizokuwa zimesambazwa mitandaoni,” akasema.

Bw Kainga alisema kwamba maafisa wa polisi walifika mahali hapo na wakamtia mbaroni na baada ya kuwasiliana na wenzao kutoka Murang’a na kuthibitisha uhalisia wa mshukiwa huyo kuwa anayesakwa, akafungiwa.

“Kwa sasa mipango inafanywa ya kumsafirisha mshukiwa huyo hadi Kaunti ya Murang’a ambapo tutamhoji tukiandika taarifa yake na hatimaye tuafikie uamuzi kuhusu mashtaka,” akasema Bw Kainga.

Mnamo Desemba 20, 2023, watoto wa mwalimu huyo wakitambuliwa kama Roy Irungu wa umri wa miaka mitano na Joseph Karanja aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu, walipatikana nyumbani kwake katika kijiji cha Kieni kilichoko eneobunge la Kiharu wakiwa wamelala kwa damu yao kitandani.

Waandishi wa habari wakiwa katika boma la mwalimu James Gitau Karanja ambaye ameenda mafichoni baada ya kuwachinja watoto wake wawili na kuwaua. PICHA | MWANGI MUIRURI

Wote walikuwa wamekatwa shingoni.

“Ripoti ya upelelezi inaonyesha kwamba mke wa mshukiwa akijulikana kama Muthoni Gitau, alikuwa amemuacha miezi miwili iliyopita baada ya mzozo wa kinyumbani na akamwachia watoto hao,” akasema Bw Kainga.

Hatimaye, majirani baada ya kuingiwa na shaka ya kukosa kuona watoto hao walitekeleza uchunguzi wao na ndipo juhudi zilizoshirikishwa na chifu wa eneo hilo Bw Jason Hiuhu zikaishia kuwapata watoto hao wakiwa wamechinjwa shingoni na kuaga dunia ndani ya nyumba yao.

Bw Kainga alisema kwamba “kufikia sasa bado mshukiwa mkuu wa ukatili huo ni baba yao na ambaye sasa tutamhoji akifikishwa hapa Murang’a ndipo tupate mwelekeo katika juhudi za kusaka haki”.

  • Tags

You can share this post!

Natalie: Niliachwa kwa sababu ya maradhi

Sniper: Ripoti ya uchunguzi wa awali yatoka

T L