• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
MWALIMU: Siri yake darasani iko katika nyimbo

MWALIMU: Siri yake darasani iko katika nyimbo

NA CHRIS ADUNGO

KINACHOMTOFAUTISHA Bw George Kinyua na walimu wengine ni upekee na wepesi wake wa kutunga nyimbo rahisi zinazowezesha wanafunzi kukumbuka hoja muhimu katika mada mbalimbali za masomo anayofundisha kwa sasa shuleni Premese Makueni.

“Nyimbo hufanya wanafunzi kuelewa mambo haraka, huwapa hamu ya kujifunza vitu vipya na huwafanya kutosahau wanachofundishwa. Pia ni mbinu inayowapa baadhi yao majukwaa mwafaka ya kutambua na kutononoa vipaji vyao,” anasema.

Kwa mtazamo wa Bw George, matumizi ya nyimbo na vifaa vya kidijitali darasani husisimua wanafunzi.

Video, michoro na picha za rangi pia hufanya vipindi vya masomo kuwa vya kuvutia na hukuza ubunifu wa kiteknolojia ndani na nje ya mazingira ya shuleni.

“Kuzoesha wanafunzi kutumia vyombo anuwai vya kiteknolojia huwapa fursa ya kufanya mambo kwa kujiamini zaidi. Mbali na kuimarisha uelewa wa dhana mbalimbali, wao huanza kuona vitu wanavyofundishwa vikiwa vya kawaida mno.”

“Isitoshe, mawanda ya fikira zao hupanuka kwa wepesi na maarifa wanayoyachota kwa walimu na vitabuni huwachochea kuwa wavumbuzi,” anaelezea.

Kutokana na imani hii, ipo haja kwa mwalimu kukumbatia matumizi ya mbinu za ufundishaji zitakazompa mwanafunzi nafasi murua za kushiriki kikamilifu shughuli mbalimbali za ujifunzaji ndani na nje ya darasa.

George alizaliwa mnamo 1992 katika kijiji cha Kapyego, Kaunti ya Elgeyo Marakwet. Ndiye mtoto wa pekee katika familia ya Bw Peter Kinyua na Bi Ann Kirui.

Alisomea katika shule za msingi za Kapyego (1996-2000) na Namugoi, Kaunti ya Nandi (2001-2005) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Ortum iliyoko Kapenguria, Kaunti ya Pokot Magharibi (2006-2009).

Ingawa matamanio yake yalikuwa kuwa daktari, alihiari kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Egoji, Kaunti ya Meru mnamo 2012.

Alihitimu mwaka wa 2014 na akaajiriwa na Premese Makueni kuwa mwalimu wa Kiingereza na somo la Jamii kabla ya kupokezwa mikoba ya kufundisha Kiswahili mnamo 2015.

Zaidi ya kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, alitunga mashairi mengi yaliyofana katika mashindano mbalimbali ya tamasha za kitaifa za Muziki na Drama.

Kazi hizo za kibunifu alizozisarifu kwa ufundi mkubwa, zilimpandisha katika majukwaa mbalimbali ya kutolewa kwa tuzo za uandishi na akajizolea zawadi tele za haiba kubwa.

George aliteuliwa kuwa Mwalimu Mwandamizi shuleni Premese Makueni mnamo 2016 kabla ya kuwa Naibu Mwalimu Mkuu mnamo 2017.

Alipanda ngazi kuwa Mkuu wa Walimu na kinara wa masuala ya kiakademia mnamo 2019 chini ya Mwalimu Mkuu, Bw James Chikombe.

Mbali na kuwa mwandishi maarufu wa kazi bunilizi, kubwa zaidi katika maazimio yake ni kujiendeleza kitaaluma na kuweka hai ndoto za kuwa profesa na mhadhiri wa Kiswahili katika vyuo vikuu nchini na duniani.

George anaivulia kofia familia yake inayozidi kumpa kila sababu ya kujikaza kisabuni maishani na kuiwekea taaluma yake thamani na mshabaha.

Anamstahi sana mkewe Bi Annalyce James ambaye kwa pamoja wamejaliwa mtoto Amelia Maya.

  • Tags

You can share this post!

Omanyala, Okutoyi washauri wanatenisi chipukizi jinsi ya...

Maonyesho ya kimataifa ya vitabu yarejea baada ya kutatizwa...

T L