• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 12:44 PM
MWALIMU WA WIKI: Ng’etich zaidi ya ualimu ni kocha

MWALIMU WA WIKI: Ng’etich zaidi ya ualimu ni kocha

NA CHRIS ADUNGO

MWALIMU bora anastahili kuwa kielelezo chema kwa wanafunzi wake.

Awahimize mara kwa mara katika safari ya elimu na awachochee kujitahidi masomoni ili wazifikie ndoto zao.

Anatakiwa pia kuwa karibu na wanafunzi wake, atambue changamoto wanazozipitia, aelewe kiwango cha mahitaji ya kila mmoja na awaamshie hamu ya kuthamini stadi za kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Julius Ng’etich ambaye kwa sasa ni Mwalimu Mwandamizi katika shule ya msingi ya Missions of Hope Girls Boarding & Mixed Day iliyoko eneo la Joska, Kaunti ya Machakos.

“Mbali na kuongoza wanafunzi kufikia malengo yao ya kiakademia, mwalimu anapaswa pia kuwa mlezi wa vipaji vya watoto, rafiki wa karibu na mshauri wao kuhusu masuala mbalimbali maishani,” anasema.

“Mwalimu anayejali maslahi ya wanafunzi anastahili kujiandaa ipasavyo kwa somo lake. Ajitahidi kuhudhuria vipindi vyote na asome kutoka kwa vyanzo mbalimbali ili awe chemchemi ya maarifa kwa wanafunzi wanaomtegemea,” anasisitiza.

Ngetich alilelewa katika kijiji cha Emom, eneo la Tenges, Kaunti ya Baringo.

Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watatu wa marehemu Bw Samuel Kokwee na Bi Miriam Jerono.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Emom (1998–2006) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Kabimoi Boys, eneo la Eldama Ravine, Baringo (2007–2010).

Ingawa ndoto yake ilikuwa kusomea uhandisi, alihiari kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Nakuru (2012–2014).

Aliyemchochea zaidi kujibwaga katika ulingo wa ualimu ni ami yake, Bw Joseph Kokwee, ambaye sasa ni Mwalimu Mkuu katika shule ya upili ya Sochoi Boys, Kaunti ya Nandi.

Baada ya kuhitimu ualimu mnamo Julai 2014, Ng’etich alianza kufundisha katika shule ya msingi ya Soy Emining Academy iliyoko Mogotio, Baringo.

Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka mitatu na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi kabla ya kuhamia shule ya msingi ya Tenges mnamo Januari 2018.

Ilikuwa hadi Januari 2021 ambapo aliajiriwa na shule ya Missions of Hope kufundisha Kiswahili, Hisabati na somo la Jamii. Alipanda cheo kuwa Mwalimu Mwandamizi mnamo Juni 2022.

Zaidi ya kufundisha, Ng’etich pia ni kocha wa handiboli – mchezo uliowahi kumpa fursa ya kuwakilisha shule yake ya upili hadi kiwango cha mkoa alipokuwa mwanafunzi wa Kabimoi Boys.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kujitosa katika uandishi wa kazi bunilizi na vitabu vya kiada anavyohisi vitabadilisha sura ya ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili nchini Kenya. Mbali na kuwa mhamasishaji wa Kiswahili, anapania pia kujiendeleza kitaaluma na kusomea shahada ya masuala ya usimamizi.

Ng’etich anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala walimu wengi chipukizi ambao hutangamana naye katika warsha na makongamano mbalimbali ya kielimu. Kwa pamoja na mkewe, Bi Lilian Kipyegon, wamejaliwa watoto wawili – Dylan Kipkurui na Emmanuel Kipng’eny.

Bi Kipyegon kwa sasa ni mwalimu wa Kiingereza na somo la Dini katika shule ya msingi ya Soy Emining Academy.

  • Tags

You can share this post!

Riba ya ‘Hustler Fund’ kuwa asilimia 9,...

Washikadau wa soka waunga Namwamba kuongea na FIFA

T L