• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:55 AM
Washikadau wa soka waunga Namwamba kuongea na FIFA

Washikadau wa soka waunga Namwamba kuongea na FIFA

NA CECIL ODONGO

WASHIKADAU wa soka nchini wamekaribisha uamuzi wa Waziri Mteule wa Michezo Ababu Namwamba kuzungumza na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) moja kwa moja iwapo uteuzi wake utaidhinishwa.

Namwamba alifika mbele ya Kamati ya Uteuzi Bungeni mnamo Ijumaa ambapo aliahidi kuwa kitu cha kwanza atafanya baada ya kuingia afisini ni kumpigia simu Rais wa FIFA Gianni Infantino ili marufuku ambayo Kenya inatumikia iondolewe.

“Naunga kauli ya Namwamba kuhusu kufikia FIFA moja kwa moja kwa kuwa hili ni suala ambalo linahitaji utatuzi wa haraka. Hakuna haja ya kupokea maoni kutoka kwa mtu yeyote kwa sababu wanaotaka kumshauri nao wana malengo yao ya kibinafsi,” akasema aliyekuwa mwaniaji wa Urais wa FKF Lordvick Aduda.

Afisa huyo ambaye ni Mkurugenzi wa Michezo kambini mwa Gor Mahia alimsifu Namwamba kwa kuahidi kupigania kuinuka kwa mchezo huo ambao unahusudiwa sana nchini. Aduda alimtaka Namwamba ahakikishe kuwa marufuku Kenya iliwekewa inaondolewa ila kupitia kufuatwa kwa sheria.

Naye aliyekuwa Katibu wa Cecafa Nicholas Musonye aliwakashifu wale ambao wanafikiria kuwa ni lazima Namwamba apokee ushauri kutoka kwao, akisema wana ubinafsi kwa sababu katika soka washikadau wote ni sawa.

Tajriba

“Namwamba si mgeni kuhusu masuala haya na wale ambao wanasema lazima ashauriane nao wamepoteza dira. Lazima amekuwa akifuatilia masuala haya na anastahili aachwe atekeleze majukumu yake iwapo uteuzi wake utaidhinishwa,” akasema Musonye.

Mwanahabari Milton Nyakundi ambaye amekuwa akijihusisha sana na masuala ya uongozi wa soka, naye alimpongeza Namwamba kwa kusema atashauriana na Fifa ila akamwonya dhidi ya kumrejesha uongozini aliyekuwa Rais wa FKF Nick Mwendwa.

“Hili si jambo rahisi kwa sababu Nick Mwendwa na kundi lake wanataka serikali hii iwajumuishe katika usimamizi wa soka. Hili ni suala ambalo hatutalikubali kamwe. Namwamba anastahili kuzungumza na Fifa mwenyewe na kutupa mwelekeo badala ya kushauriana na watu ambao wamerejesha nyuma soka yetu,” akasema Nyakundi.

Mwenyekiti wa vuguvu la timu za Ligi Kuu (KPL) Ray Oruo naye alisema Namwamba alionyesha hekima jinsi alivyoahidi kuongoza wizara hiyo na anastahili kupewa nafasi mwenyewe atokomeza utata huo wa Fifa.

“Hapa tuna siasa zetu za mpira na akishauriana nasi kabla ya kuelekea Fifa atachanganyikiwa zaidi. Anastahili kufuata sheria na kuzungumza na Fifa ili marufuku hiyo iondolewe kabla ya Kombe la Dunia kuanza,” akasema Oruo.

Afisa huyo kwa mara nyingine alishikilia kuwa timu za KPL hazitashiriki msimu mpya kabla ya marufuku hiyo ambayo Kenya iliangushiwa mnamo Februari 24, 2022 haitaondolewa.

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Ng’etich zaidi ya ualimu ni kocha

PAUKWA: Ndovu kabomoa nyumba, majirani wamsaka Tundu

T L