• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Mwanablogu wa Jubilee asimulia alivyopoteza ujauzito wa mapacha

Mwanablogu wa Jubilee asimulia alivyopoteza ujauzito wa mapacha

NA SAMMY WAWERU

MWANABLOGU wa chama cha Jubilee Pauline Njoroge amesimulia jinsi alivyopoteza ujauzito wa mapacha, hatua iliyomsawijisha moyo.

Hata ingawa hajafichua mwaka aliopitia hali hiyo, Bi Pauline kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook amesema haikuwa rahisi kusahahu tukio hilo.

Pauline alitoa ushuhuda huo Sikukuu kuadhimisha siku ya Mama Duniani, Mei 14, 2023.

“Kupoteza watoto wangu hata kabla hawajazaliwa ilinifisha moyo, hasa kuona wakipotea kupitia mkondo wa damu iliyosambaa ilisababishia uchungu usiomithilika,” aliandika.

Kwa mujibu wa masimulizi yake, aliashiria kupoteza ujauzito wake kupitia kuharibika kwa mimba (miscarriage).

Haikuwa muda mrefu kutoka sasa, nilikuwa nimebeba mapacha na walinipa furaha tele maishani, Pauline alielezea.

Kupitia chapisho hilo, mwanablogu huyo alielezea ujauzito wa watoto hao ulivyomletea furaha maishani kiasi cha rafikiye wa karibu kumpa jina la utani Mama Furaha.

Liliandamana na picha anayoonekana akipakata ujauzito, huku akiwa anatabasamu.

“Kwa muda wa miezi kadha baada ya tukio hilo, nilisawijika na hakuna jambo ambalo lingenituliza. Nilimwaga machozi mara milioni moja, yakawa (machozi) chakula changu cha kila siku,” Pauline alikumbuka, akisimulia jinsi alivyojipa nguvu na ujasiri akiwa kwenye umma licha ya uchungu aliopitia.

“Hata hivyo, ninafurahia kufuatia mtandao wa wasaidizi walioingilia kati na kunisaidia kustahimili machungu niliyopitia na zaidi ya yote Mungu kunifariji.”

Pauline aidha alitakia kila la heri kina mama wote, akisema ni baraka kubeba kiumbe na kukileta duniani.

Chini ya utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Pauline alikuwa miongoni mwa waliotetea serikali kwa hali na mali mitandaoni kupitia uanaharakati na uanablogu wake.

  • Tags

You can share this post!

Rigathi atetea ukabila katika uteuzi serikalini

Hofu ya familia kufurushwa makwao, mimea ikinyunyiziwa...

T L