• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Rigathi atetea ukabila katika uteuzi serikalini

Rigathi atetea ukabila katika uteuzi serikalini

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Rigathi Gachagua mnamo Jumamosi aliendelea kutetea mtindo wa kupendelea makabila fulani katika teuzi za maafisa wakuu serikalini akisema unaakisi jinsi watu wa makabila hayo walipiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita.

Akiongea wakati wa mazishi ya Mama Mukami Kimathi, katika eneo la Njambini, kaunti ya Nyandarua, Bw Gachagua alimpongeza Rais William Ruto kwa kuteua idadi kubwa ya watu kutoka jamii ya Agikuyu serikalini akisema “hii ni haki yetu.”

Alisema watu wa jamii hiyo, anakotoka, ndio wengi nchini na walimpigia Dkt Ruto kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 hivyo hamna kosa lolote kwa wengi wao kutunukiwa nyadhifa nyingi serikalini.

“Juzi, nimesoma magazetini watu wengine walipiga kelele kwamba umeteua Wakikuyu wengi katika serikali yako. Sasa nauliza kuna kosa gani tukiwa wengi katika serikali ya Ruto tuliopigia kura kwa wingi?” Bw Gachagua akauliza.

“Wale wanadai tuko wengi serikalini wajue pia tuko wengi katika gereza la Kamiti. Kwa nini hawasemi watu wetu waachiliwe huru twende nyumbani?” akaongeza.

Bw Gachagua alisema watu wa jamii hiyo wanashikilia vyeo vikuu serikali kwa misingi ya uamuzi wa kumpigia Dkt Ruto kura kuwa Rais.

“Wakikuyu ni wachapa kazi na ndio maana waliamua kukupigia kura kwa sababu wewe ni mchapa kazi na unazo sifa zote za kuendesha taifa hili katika mkondo wa ufanisi. Wale wanaolalamika walipiga kura upande ule mwingine na tukashinda kwa njia ya haki,” akaongeza huku akimtaka Dkt Ruto kuendelea kuteua watu wengi kutoka jamii ya Agikuyu katika serikali yake ya Kenya Kwanza.

Naibu Rais alikuwa akirejelea wito wa viongozi wa makanisa nchini waliolalamikia kile walichokitaja kama mtindo wa Rais Ruto kupendelea jamii ya Agikuyu na Kalenjin katika teuzi za wanaoshikilia nyadhifa kuu serikalini na mashirika yake.

  • Tags

You can share this post!

Fahamu asparaga na faida zake kwa mwili

Mwanablogu wa Jubilee asimulia alivyopoteza ujauzito wa...

T L