• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
NASAHA ZA RAMADHAN: Tuwafunze watoto kujaribu ibada ya saum wakiwa wangali wadogo

NASAHA ZA RAMADHAN: Tuwafunze watoto kujaribu ibada ya saum wakiwa wangali wadogo

Na NURU SAID

NEEMA kubwa ya ndoa ni kubarikiwa kupata watoto. Kila mmoja hufanya juhudi angalau amtafute mume au mke mwema ili apate kizazi chema.

Mtoto anapozaliwa, miongoni mwa mambo ya kidini yatakayomfanya kuwa mwema ni kujifunza ibada.

Haiwezekani mtu kuanza kufanya ibada akiwa mkubwa bila ya kuanza na mazoezi.

Mtume Muhammad (SAW) amelizungumzia hili kwa kusema, “Wafunzeni watoto wenu kuswali wakiwa na umri wa miaka saba, na muwachape wakifisha miaka kumi.”

Kauli yake ni wazi kwamba ibada zote lazima zianze kuwekwa ndani ya kifua cha mtoto kuanzia akiwa na umri wa miaka saba na akikaidi akifika miaka kumi, basi una ruhusa ya kumuadhibu.

Wazazi wengi huona huo huwa umri ambapo mtoto bado ni mdogo na hana uwezo wa kufunga kikamilifu. Katika umri huu, mtoto hupenda sana kubembelezwa na kusifiwa. Ikiwa utamsifu kwa kujaribu kufunga, basi ataweza. Mhimize aanze kufunga angalau mpaka saa nne asubuhi kisha unampa chai wamwambia hiyo ndiyo futari yake.

Akisonga songa mfikishe adhuhuri kisha mwambie afuturu. Siku nyingine mfikishe alasiri na mwishowe utamuona atataka kufika magharibi kama wewe mtu mzima.

Unapofanya haya yote, mpe ahadi ya zawadi. Mwambie akimaliza kufunga siku zote basi utamnunulia nguo nzuri za Iddi na utampeleka sehemu nzuri nzuri akasherehekee na kadhalika. Utashangaa akifikisha miaka kumi, huyo mtoto atafunga Ramadhani nzima.

Pia usisahau kuwahimiza watoto kuamkia daku. Nakumbuka nilipokuwa mdogo hakuna kilichokuwa kinanipa faraja kama kuamka na watu wazima wakati wa kula daku.

Ili mtu awe mzazi mwema, yampasa aache uzembe, huruma, kubembeleza na yeye mwenyewe kutofunga. Kufanya hivyo kutawatoa watoto kutoka kwa ibada. Watachukulia kufunga kuwa ni balaa na mara nyingine muhali kabisa. Tuweni wazazi wema. Tuwajenge watoto wetu imani zao. Tuzitie saum katika nyoyo zao.

You can share this post!

Al Duhail yatoka sare na Al Ahli Saudi kwenye Klabu Bingwa...

MAKALA MAALUM: Wamaragoli wanaoishi Uganda watarajiwa...