• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Al Duhail yatoka sare na Al Ahli Saudi kwenye Klabu Bingwa Asia

Al Duhail yatoka sare na Al Ahli Saudi kwenye Klabu Bingwa Asia

Na GEOFFREY ANENE

“BAHATI mbaya tuliambulia alama moja pekee. Hata hivyo, bado kuna alama nyingi za kupigania.”

Hayo ni maneno ya Michael “Engineer” Olunga akielezea masikitiko yake baada ya timu yake ya Al Duhail kutupa uongozi dakika ya mwisho katika sare ya 1-1 dhidi ya wenyeji Al Ahli Saudi kwenye Klabu Bingwa bara Asia mnamo Jumapili usiku.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alifunga bao la miamba hao wa Qatar dakika ya 53.

Olunga, ambaye hakuwa amefunga bao kwenye mashindano yoyote ya Klabu Bingwa, alipachika goli hilo kwa kukamilisha kwa ustadi krosi kutoka kwa kiungo Edmilson Junior. Alisukuma shuti kali ndani ya kisanduku hadi wavuni akitumia mguu wake wa kulia.

Al Duhail ilionekana kuwa mbioni kuzoa ushindi wake wa pili mfululizo baada ya kuchabanga Al Shorta kutoka Iraq 2-0 katika mechi yake ya ufunguzi Aprili 15. Hata hivyo, dakika sita baada ya kupumzisha Olunga, Omar Al Somah alisawazishia Al Ahli kutokana na pasi ya Motaz Hawsawi.

Vijana wa Sabri Lamouchi wanashikilia nafasi ya pili kwenye Kundi C kwa alama nne. Esteghlal kutoka Iran imekalia juu ya jedwali baada ya kubwaga Al Shorta 3-0 Jumapili. Ilikuwa imefungua kampeni yake kwa kupepeta A Ahli 5-2 katika siku ya kwanza.

Al Duhail itakabiliana na Esteghlal katika mchuano wake ujao mnamo Aprili 21.

Kabla ya kujiunga na Al Duhail, Olunga alikuwa ameshiriki Klabu Bingwa akiwa bado anashiriki Ligi Kuu ya Kenya. Alisakata michuano miwili ya Klabu Bingwa Afrika akiwa Tusker FC dhidi ya miamba wa Misri, Al Ahly katika raundi ya kwanza mwaka 2013. Pia, alichezea Gor Mahia mechi mbili za raundi ya kwanza dhidi ya AC Leopards mwaka 2015. Hakufunga bao katika michuano hiyo minne ambayo Tusker na Gor zilipoteza.

Alikaribia kupata goli la kwanza kwenye Klabu Bingwa dhidi ya Shorta wakati shuti lake liliguswa na beki Hussam Kadhim.

You can share this post!

Kipchoge afagia NN Marathon, macho sasa kwa Olimpiki

NASAHA ZA RAMADHAN: Tuwafunze watoto kujaribu ibada ya saum...