• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
NDIVYO SIVYO: Matumizi yaliyozoeleka ya kauli ‘kwa mpigo’ ni potoshi

NDIVYO SIVYO: Matumizi yaliyozoeleka ya kauli ‘kwa mpigo’ ni potoshi

NA ENOCK NYARIKI

KATIKA mazungumzo, kauli ‘kwa mpigo’ hutumiwa kwa maana ya ushindi mkuu au ushindi usiotarajiwa.

Hivi ndivyo baadhi ya watu walivyozoea kuitumia.

Licha ya maana ya msingi ya msamiati wowote, maana nyingine hujitokeza katika miktadha ya matumizi.

Miktadha hiyo inaweza kuwa ya mazungumzo au andishi.

Kwa hivyo, mojawapo ya maana za kauli ‘kwa mpigo’, kwa mujibu wa jamii linamotumiwa, ni ushindi au bahati nasibu.

Hata hivyo, katika makala haya tutaangazia maana ya msingi ya dhana mpigo na maana inayoibuliwa nayo katika kauli tuliyoitaja ili kuipambanua.

‘Mpigo’ ni neno ambalo limeundwa kutokana na kitenzi piga. Dhana hiyo ina maana ya jinsi ya upigaji ala ya muziki aghalabu ngoma.

Neno jingine linalotokana na kitenzi piga ni ‘kipigo’ lenye maana ya kichapo kinachoelekezwa kwa mtu au mnyama. Matumizi ya neno hili hukusudiwa kuchora taswira ya ukatili.

Neno mpigo pia huibua dhana ya wakati mmoja au wakati sawa. Waama, vyombo vya habari vililitumia neno hili kuelezea kitendo cha mzazi kuzaa watoto watatu au zaidi kwa wakati mmoja. Kwa hivyo, utamsikia mtu akisema, ‘amejifungua watoto watatu kwa mpigo’ akiwa na maana kuwa watoto hao wamezaliwa wakati mmoja.

Alhasili, baadhi ya watu hasa watangazaji huutumia msemo ‘kwa mpigo’ kuelezea ushindi mkubwa au wa bahati nasibu. Ifahamike hata hivyo kwamba maana ya msingi ya msemo huo ni utokeaji wa jambo kwa wakati mmoja.

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Mabunge ya Kenya yatuzwa na chama cha...

Muyoti aanza kupanga City Stars upya

T L