• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 2:00 PM
ONYANGO: Vyama vya kikabila si kichocheo cha maendeleo

ONYANGO: Vyama vya kikabila si kichocheo cha maendeleo

Na LEONARD ONYANGO

WANASIASA wameanza kucheza ngoma ya ukabila huku Uchaguzi Mkuu wa 2022 ukikaribia.

Miito ya kuunda vyama vya kisiasa ‘vitakavyotetea’ masilahi ya makabila au maeneo fulani imetapakaa kila kona ya nchi.

Kwa mfano, mapema Julai, mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing, alitangaza kuwa jamii ya Wapokot itaunda chama cha kisiasa kitakachoongozwa na Gavana wa Pokot Magharibi John Lonyangapuo.

Bw Pkosing aliyekuwa akihutubia wanahabari mjini Kapenguria alisema kuwa watatumia chama hicho ‘kupigania’ masilahi ya jamii ya Wapokot.

Viongozi wa eneo la Pwani pia wamekuwa wakijadili suala la kutaka kuunda chama watakachotumia ‘kutetea’ masilahi yao.

Aprili mwaka huu, viongozi kutoka eneo la Meru wakiongozwa na Gavana wa Kaunti hiyo Kiraitu Murungi na mbunge wa Imenti Kaskazini Rahim Dawood, walitangaza kuwa wataunda chama kitakachotetea masilahi ya jamii ya Wameru na wakazi wa eneo la Mlima Kenya Mashariki.

Ripoti za vyombo vya habari pia zinadai kuwa waziri wa Ugatuzi Eugine Wamalwa tayari amezindua chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) – kilicho na nembo yam bolea – atakachotumia kuwania ugavana wa Kaunti ya Trans Nzoia na ‘kupigania’ masilahi ya wakazi wa eneo hilo.

Hiyo ni mifano michache tu ya vyama vya kisiasa ambavyo wanasiasa waahadaa Wakenya kwamba watavitumia kupigania masilahi yao.

Kwanza, vyama vya aina hii vinakiuka Katiba. Kulingana na Kifungu cha 91(1) cha Katiba, chama cha kisiasa ni sharti kiwe na sura ya kitaifa. Katiba pia inataka chama cha kisiasa kuwa katika mstari wa mbele katika kutetea utangamano nchini na wala si kutetea kabila au eneo fulani.

Kifungu cha 91 (2) kinasema kuwa chama kisiundwe kwa misingi ya kikabila, lugha, rangi, eneo au jinsia.

Pili, Kenya haina uhaba wa vyama. Kulingana na takwimu za Msajili wa Vyama vya Kisiasa, kuna vyama 85 vilivyosajiliwa kuendesha shughuli za kisiasa humu nchini.

Aidha, kuna vyama 22 ambavyo vimetuma maombi ya kutaka kusajiliwa. Iwapo vyama hivyo vitasajiliwa, basi humu nchini kutakuwa na jumla ya vyama vya kisiasa 107.

Idadi hiyo ni zaidi ya mara mbili ya makabila ya humu nchini.

Tatu, wanasiasa wanatumia vyama hivyo kutetea masilahi ya matumbo yao na wala si kwa manufaa ya wananchi.

Nne, mfumo wa ugatuzi uliomo katika Katiba unalenga kuhakikisha kuwa kila eneo linapata mgao wa maendeleo bila kushibikiza kupitia vyama.

Wakenya wasikubali kulaghaiwa na wanasiasa hao wanaojitakia makuu – vyama vya kisiasa havina manufaa kwa kabila au jamii fulani bali ni mali ya wachache wanaotaka kujaza matumbo yao.

[email protected]

You can share this post!

Mashabiki wataka kocha Mikel Arteta apigwe kalamu baada ya...

NGILA: Tuwazie upya kuhusu Afrika tunayoitamani kiteknolojia