• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
NGUVU ZA HOJA: Kiswahili ni mhimili mkuu wa mshikamano wa kitaifa

NGUVU ZA HOJA: Kiswahili ni mhimili mkuu wa mshikamano wa kitaifa

NA PROF CLARA MOMANYI

MENGI yamesemwa na kuandikwa kuhusu umuhimu wa Kiswahili katika ujenzi wa umoja na mshikamano nchini.

Uradidi wa hoja hii huenda sasa unawakirihi baadhi ya wale wasiothamini Kiswahili kama lugha inayoweza kufisha kabisa tofauti zetu za kikabila, kitamaduni na hata kidini. Matopa ya vitabu yameandikwa kuhusu mada hii.

Nyimbo na tungo za mashairi zimetungwa na kukaririwa kwa siku ayami ili angalau kuyanasa masikio ya watu kuhusu ukuruba ulioko baina ya lugha na maendeleo ya jamii katika nyanja zote za maisha.

Makala na maoni mbalimbali yameandikwa na kusomwa kwenye magazeti, majarida na katika mitandao ya kijamii kuhusu matumizi ya Kiswahili katika kufanikisha maendeleo endelevu nchini Kenya.

Jambo muhimu ni kwamba katika juhudi hizi zote pamoja na raghba ya baadhi ya wasomi wa Kiswahili kuona kwamba lugha hii imechukua nafasi yake kama lugha rasmi na ya kitaifa, mwishowe tumeona mwanya wa matumaini.

Baadhi ya wabunge katika Bunge letu la kumi na tatu wameona upo umuhimu wa kuunda chombo kitakachoiwezesha lugha ya Kiswahili kutekeleza majukumu yake ya kikatiba. Chombo hicho ni Baraza la Kiswahili la Taifa.

Ijapokuwa imewachukua muda mrefu kuona faida ya kuundwa kwa baraza hili, Waswahili husema ‘kawia ufike’ na ‘mambo yafaayo watu ni yaingiayo chunguni’.

Tunampa mkono wa tahania mheshimiwa Abdi Yusuf Hassan kwa kuwasilisha Bungeni hoja ya kuundwa kwa Baraza la Kiswahili nchini. Baraza hili bila shaka litachangia pakubwa katika kuimarisha Kiswahili nchini.

Faida za baraza kama hilo ni nyingi. Kwa mfano, Kiswahili kama lugha ya kuunganisha wananchi, kuimarisha umoja na mshikamano wa taifa ni baadhi ya mambo yatakayovuviwa na baraza hilo kulingana na mahitaji ya Katiba ya nchi.

You can share this post!

Japhet Koome sasa asubiri kuapishwa rasmi kuwa Inspekta...

MIZANI YA HOJA: Ni muhimu kuwa na malengo ya kukuelekeza na...

T L