• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
NGUVU ZA HOJA: Lugha ya Kiswahili itendewe haki kwa kuongezewa vipindi

NGUVU ZA HOJA: Lugha ya Kiswahili itendewe haki kwa kuongezewa vipindi

NA PROF JOHN KOBIA

KULINGANA na Katiba ya Kenya ya 2010, lugha rasmi nchini ni Kiswahili na Kiingereza.

Hata hivyo, ukichunguza vipindi vilivyotengewa masomo mbalimbali katika mfumo wa elimu wa kiumilisi kuanzia gredi ya kwanza hadi ya saba itabainika kuwa Kiswahili kimetengewa vipindi vichache vya ufundishaji na ujifunzaji ukilinganisha na Kiingereza.

Kwa mfano, katika mgao wa vipindi katika gredi ya saba lugha ya Kiswahili imetengewa vipindi vinne katika wiki ikilinganishwa na lugha ya Kiingereza ambayo imetengewa vipindi vitano.

Hii inamaanisha kuwa huenda kuna siku ambayo wanafunzi katika daraja ya awali ya shule za sekondari hawatafunzwa au kujifunza Kiswahili darasani.

Hali hii haitendei Kiswahili haki.

Wizara ya elimu na Taasisi ya Ukuzaji Mitaala Kenya inapaswa kutendea haki lugha ya Kiswahili kwa kuongeza vipindi vya Kiswahili angalau viwe vitano katika gredi ya saba, nane na tisa.

Hii ni kwa sababu Kiswahili ni lugha rasmi na wanafunzi wanapaswa wawe na muda wa kutosha wa kujifunza stadi mbalimbali ili kukuza mawasiliano.

Vivyo hivyo, tunapendekeza katika mtaala wa gredi ya kumi hadi kumi na mbili lugha ya Kiswahili itengewe vipindi visivyopungue sita kwa wiki.

Katika nchi yoyote iwayo yenye wingilugha, lugha zina hadhi tofauti.

Kikatiba, serikali ya Kenya ina wajibu wa kuimarisha hadhi ya Kiswahili kimaksudi. Njia mojawapo ni kuhakikisha lugha ya Kiswahili inatengewa vipindi vinavyostahili katika mfumo wa elimu wa kiumilisi.

Kwa kufanya hivyo, tutakuza uzalendo kwa kuinua hadhi ya lugha ya Kiswahili kimaksudi.

  • Tags

You can share this post!

Achraf Hakimi na Wahbi Khazri miongoni mwa wawaniaji 12 wa...

Wakulima wa chai kupata bonasi ya juu ikilinganishwa na ya...

T L