• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 5:55 AM
Achraf Hakimi na Wahbi Khazri miongoni mwa wawaniaji 12 wa tuzo ya Marc-Vivien Foe

Achraf Hakimi na Wahbi Khazri miongoni mwa wawaniaji 12 wa tuzo ya Marc-Vivien Foe

Na MASHIRIKA

BEKI wa kulia wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Morocco, Achraf Hakimi na kiungo wa Saint-Etienne na timu ya taifa ya Tunisia, Wahbi Khazri ni miongoni mwa wanasoka 12 ambao wameteuliwa kuwania tuzo ya Marc-Vivien Foe 2022.

Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka kwa Mchezaji Bora wa Afrika katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Nyota wa timu ya taifa ya Mali ambaye ni nahodha wa Rennes, Hamari Traore na fowadi wa Nantes na timu ya taifa ya Nigeria, Moses Simon pia wametiwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo hiyo.

Wanasoka wengine wanaopigania tuzo hiyo Sofiane Boufal wa Angers na timu ya taifa ya Morocco, Karl Toko Ekambi wa Olympique Lyon na timu ya taifa ya Cameroon. Mshindi wa taji hilo mnamo 2021 alikuwa Gael Kakuta wa Lens na timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Tuzo hiyo hutolewa kwa heshima ya marehemu Foe aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 28 baada ya kuanguka na kuzimia ghafla uwanjani alipokuwa akichezea Cameroon dhidi ya Colo,bia mnamo 2003.

Mshindi wa tuzo hiyo huchaguliwa na wanahabari kutoka matawi yote ya vyombo vya habari nchini Ufaransa na hudhamiwa na Radio France Internationale (RFI) na runinga ya France 24.

Mbali na Hakimi, Traore, Simon na Khazri, sogora mwingine anayepigiwa upatu wa kutwaa taji hilo mwaka huu ni Idrissa Gana Gueye wa PSG na timu ya taifa ya Senegal. Mwingine ni Mario Lemina wa Nice na timu ya taifa ya Gabon. Lemina amewahi pia kusakata soka katika Ligi Kuu nchini Italia, Uingereza na Uturuki.

Beki wa Reims na timu ya taifa ya Morocco, Yunis Abdelhamid, 34, ndiye mwaniaji mkongwe zaidi wa tuzo hiyo mwaka huu. Beki wa Rennes na timu ya taifa ya Morocco, Nayef Aguerd, 26, ameteuliwa kuwania tuzo hiyo kwa mara ya kwanza.

Mohamed Bayo wa Guinea aliyeibuka mfungaji bora wa Ligue 2 mnamo 2020-21 kwa kufunga mabao 10 akivalia jezi za Clermont pia amejumuishwa katika orodha ya wawaniaji.

Seko Fofana wa Ivory Coast aliambulia nafasi ya saba mnamo 2020-21. Nyota huyo wa zamani wa Manchester City na Fulham kwa sasa ndiye nahodha wa Lens na ametiwa pia kwenye orodha ya wawaniaji wa tuzo hiyo mwaka huu.

Mshindi wa taji hilo mwaka huu atatangazwa rasmi mnamo Mei 16, 2022.

Washindi wa awali wa tuzo ya Marc-Vivien Foe:

  • 2021 – Gael Kakuta (DR Congo/Lens)
  • 2020 – Victor Osimhen (Nigeria/Lille)
  • 2019 – Nicholas Pepe (Ivory Coast/Lille)
  • 2018 – Karl Toko Ekambi (Cameroon/Angers)
  • 2017 – Jean Michael Seri (Ivory Coast/Nice)
  • 2016 – Sofiane Boufal (Morocco/Lille)
  • 2015 – Andre Ayew (Ghana/Marseille)
  • 2014 – Vincent Enyeama (Nigeria/Lille)
  • 2013 – Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon/Saint-Etienne)
  • 2012 – Younes Belhanda (Morocco/Montpellier)
  • 2011 – Gervinho (Ivory Coast/Lille)
  • 2010 – Gervinho (Ivory Coast/Lille)
  • 2009 – Marouane Chamakh (Morocco/Bordeaux)

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

‘Aliyefunga ndoa na roho mtakatifu’ ahofiwa kufariki

NGUVU ZA HOJA: Lugha ya Kiswahili itendewe haki kwa...

T L