• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
NGUVU ZA HOJA: Nafasi ya viongozi katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili

NGUVU ZA HOJA: Nafasi ya viongozi katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili

NA PROF CLARA MOMANYI

KISWAHILI kama lugha rasmi na ya taifa nchini Kenya ina nafasi kubwa ya kuenea na kustawi iwapo viongozi kwa jumla watakuwa katika mstari wa mbele kujenga ukubalifu ufaao wa kutumia lugha hii.

Neno ‘viongozi’ hapa halimaanishi viongozi wa kisiasa pekee. Ninamaanisha wale waliopewa majukumu mbalimbali ya kutoa uongozi hususan katika sekta za kijamii. Hawa ni pamoja na viongozi wa kisiasa, kidini, kielimu, kiserikali na wale walio katika sekta nyingine mbalimbali za kijamii.

Viongozi wa namna hii wana nafasi kubwa ya kutoa mwelekeo, kuimarisha sera madhubuti za lugha, kuweka mikakati ya kuikuza na kuiboresha lugha hii kupitia kwa uundaji wa taasisi husika pamoja na ushirikishwaji wa wananchi kwa ujumla.

Kwa mfano, kupitia kwa nafasi yao katika jamii na ushawishi mkubwa wa viongozi wa kisiasa, Kiswahili kinaweza kuimarika na kuchukua nafasi yake kinayostahili nchini. Kupitia kwa ushawishi wao pia, tungekuwa sasa tuna vyombo muafaka vya ukuzaji wa lugha hii nchini. Kufikia sasa, Kiswahili kimesalia kuwa lugha rasmi kimaandishi kutokana na ukosefu wa sera muafaka za kukifanya kuchukua nafasi yake katika jamii.

Aidha, hatuoni viongozi wa kisiasa, wa kidini na hata wale walio mamlakani serikalini wakijishughulisha na kuweka mikakati ya kuimarisha sera muafaka za lugha nchini kwa ujumla. Viongozi wa kisiasa aghalabu hutumia Kiswahili katika hadhara za kisiasa, hususan wakati huu wa kitimutimu cha siasa za uchaguzi mkuu.

Mfumo wa elimu ya CBC pia una nafasi kubwa ya kuikuza lugha hii nchini kupitia kwa mwelekeo wake wa kuzingatia umilisi wa wanafunzi. Hata hivyo, tuna matumaini makubwa kwamba serikali mpya ijayo itaweka mikakati muafaka ya kukipa Kiswahili urasmi unaohitajika nchini.

  • Tags

You can share this post!

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kongamano la kuandaa Siku ya...

NGUVU ZA HOJA: Dhima ya tafsiri katika kukuza fasihi na...

T L