• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 7:55 PM
NGUVU ZA HOJA: Vyuo anuwai vitumie sasa Kiswahili kufunzia kozi ya ‘Mbinu za Mawasiliano’

NGUVU ZA HOJA: Vyuo anuwai vitumie sasa Kiswahili kufunzia kozi ya ‘Mbinu za Mawasiliano’

NA PROF JOHN KOBIA

HIVI majuzi nilisoma tangazo la kozi mbalimbali zinazotolewa na Chuo cha Mafunzo ya Utabibu cha Kenya (Kenya Medical Training College).

Kilichonivutia zaidi ni mahitaji ya kujiunga na chuo hicho ambapo mwanafunzi alihitajika kupita kwa alama fulani katika Kiingereza au Kiswahili.

Hatua hii inapaswa kupongezwa kwa sababu inaipa Kiswahili hadhi sawa na Kiingereza inavyostahili. Vyuo vingine vinapaswa kuiga mfano wa Chuo cha Mafunzo ya Utabibu cha Kenya na kukubali wanafunzi kujiunga iwapo amepita katika Kiingereza au Kiswahili.

Kwa hakika Katiba ya Kenya ya 2010 inatambua Kiswahili kuwa lugha rasmi pamoja na Kiingereza. Isitoshe, katiba hiyo inatambua Kiswahili kuwa lugha ya taifa na mawasiliano mapana.

Dhima mojawapo ya lugha ni kuwasiliana. Ni ukweli kwamba wanaopata mafunzo katika vyuo mbalimbali wanapaswa kuwa na umilisi wa Kiswahili ili waweze kuwasiliana na wananchi.

Kiswahili ni lugha ya wananchi nchini Kenya na hutumiwa na watu wa tabaka mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kitamaduni.

Chuo cha Utabibu cha Kenya hutoa mafunzo ya utabibu, upasuaji, ufamasia, uuguzi, afya ya umma na mengineyo. Wanaohitimu kutoka chuo hicho hutarajiwa kufanya kazi popote nchini Kenya.

Wataalamu hao hutarajiwa kuwasiliana na umma kwa kutumia Kiswahili. Mtaala wa kiumilisi unasisitiza ukuzaji wa umilisi wa mawasiliano katika nyanja zote za maisha ya binadamu.

Katika baadhi ya vyuo anuwai, kozi ya mbinu za mawasiliano hutolewa kwa Kiingereza.

Ni muhimu vyuo vya kiufundi na vinginevyo vitoe mafunzo ya mbinu za mawasiliano kwa Kiswahili ili wanaohitimu waweze kuwasiliana ipasavyo na wananchi.

  • Tags

You can share this post!

Vipusa wa Man-City wadengua mabingwa watetezi Manchester...

Matano alia refa alipendelea Gor, Nzoia ikisalia juu

T L