• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
‘Nililazimika kuacha shule nikaolewa, nikazaa watoto watatu, nikarejea na bado nimewika KCPE’

‘Nililazimika kuacha shule nikaolewa, nikazaa watoto watatu, nikarejea na bado nimewika KCPE’

NA JOHN NJOROGE

Baada ya kuacha shule kwa miaka saba, Bi Olivia Chepngeno hakuweza kuficha furaha yake matokeo ya KCPE 2023 yalipotolewa na Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu.

Ilikuwa ya kishindo katika Kituo cha Elimu cha Imani huko Elburgon, Kaunti ya Nakuru huku walimu, wazazi na wanafunzi wakisakata densi katika sherehe kufuatia matokeo mazuri ya darasa la 2023.

Bi Chepngeno, 23, mama wa watoto watatu alikuwa mwingi wa tabasamu wakati Taifa Leo ilipomtembelea shule alikofanyia mtihani huo.

“Niliacha shule nilipoolewa miaka saba iliyopita nikiwa Darasa la Saba. Kwa kuwa nilikuwa mwerevu na nilikuwa na uwezo wa kufanya vyema, nilishauriana na mume wangu miaka kadhaa iliyopita na kumuuliza ikiwa ningeweza kurudi shuleni na kuendelea na masomo yangu,” anakumbuka Bi Chepngeno ambaye alikuja kuwa mwanafunzi wa pili shuleni baada ya kupata alama 328,  nyuma kidogo ya mwanafunzi bora aliyepata alama 377.

Olivia Chepngeno, 23, mama wa watoto watatu aliyepata alama 328 katika Imani Educational Center mjini Elburgon, Kaunti ya Nakuru asherehekewa na walimu, wazazi na wanafunzi shuleni humo mnamo Novemba 25, 2023. PICHA|JOHN NJOROGE

Baada ya mumewe kukubali ombi lake, Chepngeno alimwendea msimamizi wa shule hiyo na kumuuliza ikiwa angejisajili kwa mtihani huo kisha arudi nyumbani na kukaa na watoto wake.

“Alikuja ofisini kwangu Machi mwaka huu akiuliza ikiwa angejiandikisha kwa mtihani wa kitaifa na kurejea kwa familia yake.  Aliposimulia hadithi yake baada ya kusajiliwa kama mtahiniwa wa mwisho, niliona uwezo wake kwani alisema alitaka kupata nafasi sekondari na kuendelea na masomo yake,” akasema Bi Rose Kirui, meneja wa shule hiyo, akiongeza kwamba baada ya mahojiano mafupi, mwanafunzi huyo alipata alama 253 na ndipo alipogundua kuwa mama huyo angeweza kufanya vyema iwapo atapewa nafasi nyingine ya masomo.

“Nilichukua muda kumwelekeza na kumshauri kwa sababu nilijua kuwa mwanamke aliyeolewa haikuwa rahisi kwake kuwa mwanafunzi wa kawaida. Wakati fulani, nilimpigia simu mumewe kwa vile sikutaka kuvunja ndoa yao kwa kumkubali mama awe shuleni bila idhini yake,” akasema Bi Kirui na kuongeza kuwa mume alikubali mkewe kuwa shuleni mara kwa mara.

Bi Kirui pia aliahidi kumnunulia sare za shule na akaanza kufika shuleni mara moja.

Katika siku zake za kwanza shuleni, Chepngeno alifichua kwamba aliona ni jambo la ajabu kuwa shuleni pamoja na watoto wake walio katika darasa la pili (miaka 7), mzaliwa wa pili katika PP2 (miaka 4) na mtoto wa tatu kuzaliwa mwenye umri wa miaka miwili.

“Ninahusisha mafanikio yangu kwa mume wangu, walimu, meneja na wanafunzi wenzangu ambao walipenda, kushirikiana na kunitendea kama wanafunzi wengine.  Kadiri wakati ulivyosonga, nilizoea na kuhisi kwamba nilikuwa mahali pazuri,” alisema Chepngeno, akiongeza kuwa alicheza nao na kushiriki katika shughuli nyingine za mtaala kama vile riadha, kuruka kamba, kandanda miongoni mwa zingine.

Chepngeno anasema kufanya kazi kwa bidii na kumtegemea Mungu pia kulichangia mafanikio yake.  Alisema masomo ya alasiri yangeisha saa kumi jioni, kisha kwenda nyumbani umbali wa mita chache kutoka shuleni ili kuandaa chakula cha jioni kwa ajili ya familia kabla ya kurejea kwa maandalizi ya jioni hadi saa tatu usiku.

Mume wake ambaye alimwita kama mume anayejali na mwenye upendo alifika kwa wakati kumchukua kila siku baada ya maandalizi ya jioni.

Akiwa ametulia na mwenye haya, anatumai kujiunga na Kipsigis Girls kwa elimu yake ya upili kisha aendee digrii yake katika Chuo Kikuu cha Kenyatta na kuhakikisha kuwa ndoto yake ya kuwa daktari inatimia.

Bi Kirui, mwalimu mstaafu alibainisha kuwa aliifanya shule iwe fahari na kumsifu kwani hajawahi kutoka shuleni hata siku moja. Alisema Bi Chepngeno amekuwa na nidhamu na hakujichukulia kama mama bali kama msichana wa shule.

“Alifanya kila awezalo na hakuna mtu ambaye angemtofautisha na wanafunzi wengine ama darasani au uwanjani. Tunatoa wito kwa watu wenye mapenzi mema kumuunga mkono kwa kuwa ana uwezo wa kufanya vyema maishani,” akaongeza Bi Kirui.

Msichana huyo aliomba usaidizi kutoka kwa wahisani ili afaulu kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka ujao kwa kuwa mumewe anafanya kazi za mkono eneo hilo.

Kumlipia karo yeye na watoto wake ilikuwa changamoto kubwa ambayo familia ilipitia lakini alishukuru uongozi kwa kumlipia karo ya shule.

Alitoa wito kwa wazazi wengine walioolewa mapema kama yeye kurejea shuleni na kutekeleza ndoto zao kwani kuolewa sio mwisho wa maisha.

  • Tags

You can share this post!

Yupo jamaa anayenipa zawadi nyingi ila simtaki

Bila shamba la ekari 50 hutamuoa Awinja, waume wanaommezea...

T L