• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2024 7:23 PM
NJENJE: M-Pesa sasa kutumika katika nchi 200 duniani baada ya kutia mkataba na kampuni ya Visa

NJENJE: M-Pesa sasa kutumika katika nchi 200 duniani baada ya kutia mkataba na kampuni ya Visa

NA WANDERI KAMAU

MAMILIONI ya wateja wa M-Pesa nchini sasa wana nafasi kulipia bidhaa na huduma katika zaidi ya nchi 200 duniani, baada ya kampuni ya Safaricom kutia saini mkataba wa kibiashara na kampuni ya Visa.

Safaricom ilitia saini mkataba huo na kampuni hiyo kubuni kadi ya M-Pesa GlobalPlay Virtual card, inayowaruhusu wateja kutoa ama kutuma hadi Sh300,000 kwa siku moja.

Mkataba huo umeupandisha hadhi mfumo wa malipo wa M-Pesa kuwa kiwango sawa na majukwaa mengine ya kimataifa ya malipo duniani.

Ili kuingia kwenye mfumo huo, wateja watahitajika kubonyeza *334#, kisha sehemu ‘6’ (Lipa Na M-Pesa).

Baadaye, watabonyeza kidude ‘M-PESA GlobalPay.’

“Kwa kushirikiana na kampuni ya Visa kubuni kadi ya M-Pesa GlobalPay Visa, tunalenga kuwawezesha wateja wetu kutumia njia hii popote walipo duniani,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom, Bw Peter Ndegwa.

Kampuni hizo mbili pia zinalenga kuzindua kadi hiyo mpya katika nchi za Tanzania, DRC Congo, Msumbiji, Lesotho na Ghana.

Mkataba huo mpya pia unatarajiwa kuisaidia kampuni ya Visa kupenya kwenye soko la Afrika.

“Visa imejitolea kupanua mfumo wa malipo yake kote barani Afrika kwa kufungua soko la dunia nzima ili kumfaa kila mteja. Ushirikiano huu mpya na kampuni ya Safaricom ni hatua kubwa katika kutimiza lengo hilo,” akasema Meneja Mkuu wa kampuni hiyo ukanda wa Afrika Mashariki, Corine Mbiaketcha.

Mkataba huo pia unatarajiwa kupiga jeki mapato ya Safaricom kupitia M-Pesa, hasa baada ya mapato ya mfumo huo kushuka kwa mara ya kwanza nchini kwa muda wa miaka mitano iliyopita.

Mwaka uliopita, Safaricom ilipata mapato ya Sh82.6 bilioni kupitia M-Pesa, ikilinganishwa na mwaka 2020, ilipojipatia mapato ya Sh84.5 bilioni.

Kiwastani, Safaricom imekuwa ikipata faida ya Sh8 bilioni kila mwaka kupitia M-Pesa tangu 2018.

Safaricom imekuwa ikiweka mikakati kuboresha mfumo wa malipo kupitia njia ya kidijitali tangu 2020, baada ya watu wengi kuegemea utumaji pesa kupitia njia hiyo.

You can share this post!

Mvurya awahimiza wapigakura Kwale wachague viongozi...

CECIL ODONGO: Kinaya Ruto haamini IEBC ilhali haiongozwi na...

T L