• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 9:13 AM
NJENJE: Wafanyabiashara wadogo wafaidika chini ya mpango maalum wa kuwapatia mikopo

NJENJE: Wafanyabiashara wadogo wafaidika chini ya mpango maalum wa kuwapatia mikopo

NA WANDERI KAMAU

JUMLA ya biashara ndogo ndogo 2,190 zimepokea Sh3.3 bilioni chini ya mpango wa serikali wa kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wa kiwango cha chini katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022.

Hata hivyo, wadau wamesema biashara nyingi hazikukua kwa kasi kama ilivyotarajiwa.Kulingana na Wizara ya Fedha, walemavu, vijana na wanawake walipewa mikopo ya Sh472.2 milioni, kiwango hicho kikiwakilisha asilimia 20.1 ya fedha hizo.

Fedha hizo zimekuwa zikitolewa chini ya Mpango wa Mikopo Maalum ya Serikali (CGS).

Hata hivyo, fedha hizo bado ni kiwango kidogo katika nchi ambayo ina jumla ya wafanyabiashara wa kiwango cha kadri wale wadogo wadogo milioni saba.

Chini ya mpango huo, serikali imekuwa ikizirai benki kuwapa mikopo wafanyabiashara hao, kwa ahadi ya kuzilipa ikiwa watakosa kuirejesha.

Kulingana na takwimu zilizowasilishwa Bungeni kutoka kwa Wizara ya Fedha, wanawake 283, vijana 150 na walemavu wanane walifaidika kutokana na fedha hizo.

“Hata hivyo, ikizingatiwa kuna idadi kubwa ya biashara ndogo ndogo zinazomilikiwa na makundi hayo, kiwango cha mikopo iliyochukuliwa bado kiko chini. Kinaonyesha kuwa makundi hayo yanachukua kiwango kidogo cha mikopo,” ikaeleza ripoti.

Mpango huo ulibuniwa Desemba 2020 na serikali kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo kupata mikopo ya kiwango cha chini kukuza biashara zao.

Hilo ni kuziepusha na ugumu wa kupata mikopo kutoka benki za kawaida.Kuna benki kadhaa zilizojumuishwa na serikali kwenye mpango huo.

Aidha, kulingana na makubaliano yaliyopo baina yake na serikali, zinaweza kulipwa fidia ya hadi robo ya mkopo aliochukua mtu, ikiwa atashindwa kulipa.

Benki zilizo kwenye mpango huo ni Absa, Credit Bank, KCB Group, NCBA, Diamond Trust Bank, Stanbic Bank na Co-operative Bank.

Mfanyabiashara anaweza kukopa hadi Sh5 milioni huku muda wa malipo ukiwa miezi 36.

“Hazina ya Kitaifa itaendelea kushirikiana na mashirika ya kifedha ya kibinafsi kuhakikisha watu wengi zaidi wamefaidika,” ikaeleza.

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Muundaji mahiri wa bidhaa za aina yake

US kutoa Sh1.2b kunasa wakuu wa Al-Shabaab

T L