• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:50 AM
US kutoa Sh1.2b kunasa wakuu wa Al-Shabaab

US kutoa Sh1.2b kunasa wakuu wa Al-Shabaab

NA MASHIRIKA

WASHINGTON DC, AMERIKA

AMERIKA imetangaza kuwa itatoa zawadi ya dola milioni 10 (Sh1.2 bilioni) kwa yeyote ambaye atatoa taarifa kuhusu viongozi wakuu wa Al-Shabaab.

Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo, ilisema kuwa mtu yeyote atakayetoa taarifa itakayowezesha kudhibiti mifumo ya kidijitali ya kifedha ya kundi la Al-Shabab lenye uhusiano na Al-Qaeda, atapokea vinono.

Hii ni baada ya kundi hilo la Al-Shabaab kuongeza mashambulio katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na maeneo mengine ya nchi hiyo.

Nchi hiyo pia imeahidi kumtuza mtu yeyote atakayetoa taarifa kuhusu anakojificha kiongozi wa Al-Shabab Ahmed Diriye, naibu wake Mahad Karate na Jehada Mostafa, raia wa Amerika anayesemakana kuwa na majukumu mbalimbali katika kundi hilo.

Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo, inamhusisha Diriye na shambulio la mwaka 2020 katika kambi ya jeshi nchini Kenya, lililomuua mwanajeshi mmoja wa Amerika pamoja na wanakandarasi wawili.

Awali, Amerika ilitoa zawadi ya hadi dola milioni 6 kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu Diriye, ambaye pia anajulikana kama Abu Ubaidah.

Kwenye bango, serikali ya nchi hiyo ilisema kuwa viongozi hao wa Al-Shabaab wamehusika na mashambulio mengi ya kigaidi nchini Somalia, Kenya na mataifa jirani na kusababisha vifo vya maelfu ya watu wakiwemo raia wa Amerika.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Volker Turk, alisema kuwa zaidi ya raia 600 wameuawa mwaka huu 2022 katika mashambulio ambayo kwa kiasi kikubwa yanahusishwa na Al-Shabaab.

Kulingana na takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa, takriban watu 613 wameuawa na wengine 948 kujeruhiwa mwaka huu 2022, idadi hiyo ikiwa ni ya juu zaidi tangu mwaka 2017.

Kundi hilo, ambalo liliwekwa kwenye orodha ya makundi ya kigaidi na Amerika mnamo mwezi Machi mwaka 2008, na limekuwa likipambana kuipindua serikali inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi kwa takriban miaka 15.

Rais Hassan Sheikh Mohamud, aliyeingia madarakani mwezi Mei, aliahidi kupambana na kundi hilo, huku wanajeshi wa serikali wakionekana kupata mafanikio katika mapambano hayo kwa kuchukua udhibiti wa maeneo yaliyokuwa mikononi mwa kundi hilo kwa muda mrefu.

Mnamo Mei, Rais wa Marekani Joe Biden aliamua kutuma wanajeshi wa Amerika nchini Somalia, akiidhinisha ombi kutoka wizara ya ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon, ambayo iliuona mfumo wa kupokezana uliopendelewa na mtangulizi wake Donald Trump kuwa hatari na usiokuwa na faida.

  • Tags

You can share this post!

NJENJE: Wafanyabiashara wadogo wafaidika chini ya mpango...

TUSIJE TUKASAHAU: Sharti waziri Zacharia Njeru asafishe...

T L