• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 12:17 PM
UJASIRIAMALI: Muundaji mahiri wa bidhaa za aina yake

UJASIRIAMALI: Muundaji mahiri wa bidhaa za aina yake

NA PATRICK KILAVUKA

ANNE Mutua amekulia jasho lake kwa miaka 30, akiunda bidhaa za shanga na maarufu zaidi mikoba akitumia aina ya shanga zinazofahamika kama saramic.

Lakini kabla ya kuamua kuingilia kazi hiyo, alikuwa na matamanio ya kusomea uanahabari baada ya kufaulu vyema na kutarajiwa kujiunga na chuo kikuu.

Hata hivyo, hawakuwa na uwezo kifedha.

Hapo, ndiyo alijipata jijini Nairobi kujitafutia riziki kwani kulikuwa na ndugu zake ambao walikuwa shuleni.

Anasema bahati yake, nyota yake ya jaha ilimwandama pale ambapo alikutana na mjasirimali anayemkumbuka kama Bw Munyao ambaye alimfungulia mlango wa heri kwa kumnoa na maarifa ya kiufundi kuhusu jinsi ya kuunda vitu vya shanga kwa weledi mno.

Anasema alichukua muda mfupi sana kuelewa kwani hata mama yake alikuwa na ujuzi huo. Walikuwa wanafanyia kazi hiyo katika eneo la kuegesha magari katika barabara ya Kigali kabla ya kubomolewa baada ya miaka miwili.

Hata hivyo, hakukata tamaa kwani aliwaza na kuwazua mustakabali atakaouchukua na akaafikia kufungua kibanda kuanza kujitegemea na hajarudi nyuma kutoka zama hizo hadi sasa.

Anafanyia kazi yake soko la Maasai ambapo wao huwa na siku za kuendesha biashara katika maeneo tofauti.

Wao huwa maeneo ya Mahakama ya Upeo mnamo Jumamosi na Jumapili, soko la City na lile lililoko karibu na Bustani ya Michuki mkabala wa barabara ya Kijabe siku ya Jumanne.

Malighafi ya saramic, mbao na shanga huwa anazinunua pamoja na nyenzo nyingine zinazohitajika kuunda bidhaa zake.

Yeye huunda mikoba hiyo ya saramic na shanga yenye ukubwa tofauti, na ambayo bei yake huwa kati ya Sh500 hadi Sh2,000.

Aidha, anapopata oda hujitahidi ukucha kwa jino kuikamilisha kwa wakati ufaao akiwa na wafanyakazi watatu ambao humsaidia.

“Mbali na kuwafunza kazi wengine wengi ambao wanajitegemea, huwa nawauzia wauzaji wa rejareja na jumla au watalii hata kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook,” anasema.

Anasema kazi hii inahitaji tu kujitolea mhanga kwa bidii ya mchwa na kuwa mbunifu.

Anne Mutua akifuma mkoba kwa kutumia shanga maalum. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Hata hivyo, anaeleza kuwa changamoto katika kazi hii imekuwa kudorora kwa utalii nchini kwa kuwa watalii hawafiki maeneo ya masoko kama awali, japo wanunuzi wa nchini wameanza kuchangamkia bidhaa zao.

Pia, wao huuzia katika soko la wazi ambapo huathiriwa sana wakati wa jua na pia mvua kwani bidhaa zao hunyeshewa au kuharibika.

Angependa kuomba serikali kuwasaidia wajasiriamali kutangaza kazi zao katika masoko ya nje ya nchini kama njia mbadala ya kitega uchumi kwao na nchini pia.

Vile vile, anaomba wasaidiwe kupata soko la kudumu badala ya hali ilivyo sasa.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Jinsi apu ya Hello Tractor inavyosaidia kuendeleza...

NJENJE: Wafanyabiashara wadogo wafaidika chini ya mpango...

T L