• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Nyani wasumbufu wanaovamia kuku na kutwanga walevi barabara ya Nakuru – Nairobi  

Nyani wasumbufu wanaovamia kuku na kutwanga walevi barabara ya Nakuru – Nairobi  

NA RICHARD MAOSI

WAFUGAJI wa kuku kutoka mtaa wa Barnabas na Pipeline kwenye barabara kuu ya Nakuru -Nairobi wanaendelea kukadiria hasara kutokana na idadi kubwa ya nyani wanaozuru makazi yao kunyaka kuku au kuiba mayai.

Wengine wanaopata pigo ni wachuuzi wa njugu, matunda, soda na wauzaji vyakula kandokando mwa barabara.

Hivyo basi, sio ajabu kukumbana na baadhi yao wakitafuta wateja huku wameshika mijeledi mikononi, ambayo kwa kawaida hutumika kuwacharaza nyani wakorofi.

Kuvamia kuku

Kulingana na Alfred Kimutai mkaazi wa eneo la Gilgil, anasema nyani wamebuni njia mpya kunyatia vibanda vya kuku wakitafuta mayai.

Nyani akikimbizana na gari katika Barabara Kuu ya Nakuru-Nairobi. PICHA|RICHARD MAOSI

Kimutai ambaye ni mkulima mzoefu anasema alistaafu yapata miaka miwili iliyopita na amekuwa akitegemea ukulima kama njia ya kukidhi mahitaji yake yote.

“Lakini nimeanza kufikiri jinsi ya kubadilisha biashara kwa sababu ufugaji wa kuku karibu na misitu au vichaka hapa hauna tija,”akasema.

Kilio cha wakazi 

Alilalamikia mchana kutwa kushinda akifukuza nyani na usiku humlazimu kukaa macho.

Anaomba serikali kuu kwa Ushirikiano na Shirika la Kenya la Wanyamapori (KWS), kuwasaidia wakazi wa maeneo yaliyoathirika kulinda mali yao ili wasije wakatumbukia kwenye lindi la umaskini ikizingatiwa kuwa hali ya uchumi ni mbaya.

Nyani wasumbufu wanaowahangaisha baadhi ya wasafiri katika barabara kuu ya Nakuru-Nairobi. PICHA|RICHARD MAOSI.

Bi Jane Kihara muuzaji wa maziwa eneo la Kikopey, anasema kuwa siku moja mwanzoni mwa mwaka huu, 2023 alifungua kazi na kupata nyani wamekunywa maziwa yote na kumwaga yaliyosalia.

Nyani kutandika walevi

Kulingana na Bi Kihara, hili sio kero la wafanyibiashara tu bali pia kwa wasafiri, akisisitiza pia hii sio mara ya kwanza kwa visa kama hivi kutokea

Awali Taifa Leo Dijitali imewahi kuangazia visa ambapo nyani walikuwa wakiwatandika walevi na kuwaibia wakazi chakula.

Nyani hao wasumbufu huibia wakazi chakula na kupiga walevi kwenye mitaa ya Barut, Flamingo, Manyani na Lakeview.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Afisa aliyeangamiza mtoto Juni 12, 2022 hajaadhibiwa mwaka...

Karen Nyamu: Nilisaidia mke wa Samidoh kupata tenda 

T L