• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
ODONGO: Rais ahakikishe miradi ya Nyanza haitelekezwi

ODONGO: Rais ahakikishe miradi ya Nyanza haitelekezwi

Na CECIL ODONGO

MIRADI yote iliyozinduliwa na itazinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta eneo la Nyanza inafaa ikamilishwe kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Rais Kenyatta anatarajiwa kuongoza sherehe za Madaraka Dei kutoka Kaunti ya Kisumu kwa mara ya kwanza katika historia ya mji huo.

Kigogo wa siasa za upinzani Raila Odinga anatarajiwa kuwaongoza wanasiasa wa ODM ambao ndio wengi eneo hilo katika sherehe hizo.

Kwanza, ni jambo jema kwamba Rais Kenyatta hatimaye anaweza kuzuru eneo la Nyanza bila hofu yoyote kutokana na salamu za maridhiano kati yake na Bw Odinga mnamo Machi, 2018.

Kabla ya kura ya 2017 na 2013 ziara ya Rais eneo hili haingekosa kuzua taharuki kutokana na uhasama uliokuwepo kati yake na Bw Odinga.

Mnamo Septemba 8, 2014, makundi ya vijana yalitibua mkutano wa Rais Kenyatta mjini Migori na hata kurusha viatu kwenye jukwaa alikokuwa ameketi Rais, Gavana Okoth Obado na baadhi ya viongozi kutoka Migori.

Lilikuwa tukio la aibu ambalo bila shaka lilichochewa na ubabe wa kisiasa kati ya Rais na Bw Odinga.

Isitoshe, ghasia na maandamano yaliyoshuhudiwa baada ya kura ya marudio ya Urais 2017 pia ilizidisha uhasama kati ya viongozi hao wawili wakuu nchini.

Uhasama kati ya familia ya viongozi hao wawili hata hivyo, ulichipuka kati ya wakazi wao baada ya taifa kujinyakulia uhuru Mzee Jomo Kenyatta na aliyekuwa Makamu wake Jaramogi Oginga Odinga licha ya kushirikiana kukomboa nchi kutoka kwa utawala dhalimu wa wazungu , waligeukiana na wakawa na uhasama mkubwa.

Matukio hayo ya kihistoria na mengine wakati wa kupigania mfumo wa vyama vingi nchini na uhasama kati ya Bw Odinga na tawala zilizopita, zote, zimechangia, eneo la Nyanza kusalia nyuma kimaendeleo.

Kwa kuwa sasa kuna utulivu na Bw Odinga anaonekana kuwa sehemu ya serikali, hakikisho la pekee kuwa hili linafanyika kwa njia njema ni miradi iliyoanzishwa ikamilishwe kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Tayari mradi wa ukarabati wa Bandari ya Kisumu inaendelea vyema pamoja na ule wa reli kutoka Nakuru-Naivasha-Kisumu.

Japo mwanakandarasi anayejenga upya Uwanja wa Jomo Kenyatta anadaiwa kufanya kazi duni, ni vyema tusubiri tuone jinsi ujenzi huo utakavyokuwa baada ya mradi wenyewe kukamilika. Kazi katika uwanja wa Oginga Odinga nayo pia inaendelea kukamilika.

Hata hivyo, mradi wa kwanza wa handisheki eneo la Nyanza, mzunguko wa barabara kuu ya Ahero, bado haujakamilika tangu 2018 pamoja na kituo kikubwa cha uchumi huko Miwani.

Na si kaunti ya Kisumu pekee, miradi ya ujenzi wa barabara kadhaa katika kaunti za Homabay, Siaya na Migori ambayo imeanzishwa na serikali inafaa pia ikamilike kwa wakati.

Rais pia anafaa ahakikishe kwa serikali inaweka mbinu ya kutokomeza janga la mafuriko katika eneobunge la Nyando na maeneo mengine. Kilimo cha mpunga kisisahaulike na pia kiwanda cha pamba kijengwe.

Maono pekee ambayo Rais anafaa kuachia wakazi wa eneo hili ambalo limesalia nyuma kimaendeleo ni kuhakikisha miradi yote iliyozinduliwa inakamilika.

Pia miradi hiyo itengewe mgao kwenye bajeti ili kusizuke tatizo la ukosefu wa fedha.

You can share this post!

Mauaji: Wapenzi wa kando washukiwa

WANGARI: Masuala ya hedhi yaangaziwe kwa kina kusaidia...