• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
WANGARI: Masuala ya hedhi yaangaziwe kwa kina kusaidia wasichana

WANGARI: Masuala ya hedhi yaangaziwe kwa kina kusaidia wasichana

Na MARY WANGARI

MNAMO Ijumaa, Kenya iliungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Masuala kuhusu Hedhi Duniani huku utafiti ukidhihirisha kwamba hakuna uhamasishaji wa kutosha kuhusu afya ya hedhi nchini Kenya.

Kando na kukosa sodo, utafiti huo umeonyesha kuwa wasichana kutoka familia maskini na zile hazina kisomo hawajui kutumia vifaa vya hedhi, jinsi ya kuvitupa baada ya kuvitumia, na hata hawana ufahamu kuhusu masuala ya hedhi.

Serikali ilipoanzisha Hazina ya Makundi Yaliyotengwa kupitia afisi ya waakilishi wa kike, lengo kuu lilikuwa kuhakikisha kuwa hakuna msichana anayekosa kufika shuleni kwa kukosa sodo kutokana na ufukara.

Hata hivyo, inasikitisha mno kuwa Hazina hiyo haijetekeleza kikamilifu sera kuhusu masuala ya hedhi hasa tangu janga la Covid-19 lilipozuka mwishoni mwa 2019 na kusababisha watoto kukaa nje ya shule kwa muda mrefu.

Gonjwa hilo liliambatana na athari hasi kiuchumi ambazo zilisababisha wazazi wengi kupoteza kazi na baadhi biashara zao zikasambaratika.

Wasichana wachanga ndio waliopata makali ya janga hilo huku wengine wakishawishiwa kushiriki ngono ili waweze kupata sodo za kujisitiri wakati wa hedhi kila mwezi.

Si ajabu kwamba visa vya mimba za mapema viliongezeka pakubwa mnamo 2020 na 2021, na kusababisha wasichana wengi kuacha masomo yao.

Tatizo kuu limekuwa ukosefu wa habari mwafaka kuhusu hedhi hali ambayo huwafanya wasichana wengi wachanga kuchanganyikiwa na hata kuhadaiwa kirahisi.

Ni sharti watoto wa kike wafahamishwe kuwa kupata hedhi si jambo la aibu, uchafu au kuchukiza bali ni mchakato asilia wa kimaumbile unaoonyesha kuwa msichana anazidi kukua kutoka utotoni na kuwa mwanamke mchanga na vilevile ni ishara ya afya njema.

Inatamausha mno kuwa suala la hedhi bado ni kero kuu nchini ambapo asilimia kubwa ya wasichana bado hawawezi kumudu sodo zinazofaa.

Huku vifaa vya hedhi kama vile taulo, chupi na kadhalika vikiwa tayari ni ghali, nyakati za hedhi kwa wasichana kutoka jamii maskini ambao hawawezi hata kupata sodo, huwa ni jinamizi kuu.

Kando na kuwaathiri wasichana kisaikolojia, suala la kukosa sera mwafaka kuhusu afya ya masuala ya hedhi limechangia pia ukosefu wa usawa kijamii na kiuchumi baina ya wanawake na wanaume nchini Kenya.

Rais Uhuru Kenyatta alitia sahihi mswada wa kufanyia marekebisho Sheria ya Elimu mnamo 2017 ambayo iliagiza wasichana wote wa shule wawe wakipatiwa sodo bora za kutosha katika mpango uliotengewa Sh538 milioni.

Ni sharti serikali iharakishe kwa dharura utekelezaji wa sera kuhusu hedhi ambayo ni mchakato wa kiasilia katika maisha ya mwanamke unaohitaji kuangaziwa kwa mwelekeo jumuishi.

You can share this post!

ODONGO: Rais ahakikishe miradi ya Nyanza haitelekezwi

TAHARIRI: Vita vya Knut, TSC havifai wakati huu