• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:42 PM
Afichua siri kubwa ya wanawake wanaojiuza kimwili, akisema wengi wao huhatarisha afya zao kusudi wapate pesa

Afichua siri kubwa ya wanawake wanaojiuza kimwili, akisema wengi wao huhatarisha afya zao kusudi wapate pesa

NA FRIDAH OKACHI

KUSAKA pesa kupitia kujiuza kimwili kumesababisha wanawake wanaochukua hatua hiyo ambayo haijakubalika kimaadili, kuzuia hedhi zao kwa muda wa zaidi ya saa 12.

Carolyne Njoroge anasema amejionea mwenyewe mazingira magumu na hatari ambayo wanawake wanaojiuza kimwili hupitia.

Ingawa anasema baadhi ya wasichana hao hujiingiza kwa tabia hizo kutokana na changamoto za kidunia na kinyumbani, wakishafika katika vichochoro vya biashara hiyo yao, hulazimika kuchukua hatua zenye madhara tele kwa afya zao.

Anafichua baadhi ya wasichana hao hukiuka mfumo na utaratibu wa kimaumbile kwa kujiingiza pamba ili ‘kuzuia’ hedhi ili waendelee kujiuza kupata pesa mfululizo.

“Mimi ni mtoto wa mtaani. Mama yangu alifanya biashara ya kujiuza na aliuawa nikiwa na umri wa miaka 14. Sikujua mtu mwingine wa familia lakini ninachofahamu ni kwamba wanawake wengi wanaojiuza kimwili hupitia changamoto tele,” anasema Carolyne.

Anawashauri watoto wa mitaani, haswa wasichana, kuhakikisha wanauliza wazazi wao kuwaelezea walipo watu wengine wa familia yao kwa sababu hiyo inaweza kusaidia.

“Mwanzo nilijua ni mimi na mama. Wakati alifariki, nilianza kufanya fujo na vita kila wakati. Kila wiki nilikuwa ninapelekwa makamani. Hadi siku moja jaji akasema nisipelekwe tena,” akasema.

Carolyne anasema wanawake katika sekta hiyo tata walikiri na kumdokezea kwamba hutumia pamba kwa kuisukuma ndani zaidi siku zao za mwezi ili kuendelea na kujiuza kimwili.

Anasema licha ya wanawake wengi kuwa na maono, kwa sababu moja au nyingine hujipata wakiendelea kujihusisha na mambo ambayo huwaathiri kiafya.

“Ukweli usemwe, ni sharti mwanamke anayefanya hivyo ajue kwamba pamba inaweza ikakataa kutoka hivyo imlazimu mwathiriwa kumuendea mtaalamu wa afya,” anaeleza.

Dkt Joshua Kimani anasema pamba ikitumika kwa mazingira kama hayo humweka mwanamke katika hatari ya kupata ugonjwa wa Toxic syndrome na maambukizi ya njia ya mkojo (UTI).

“Ugongwa wa Toxic syndrome huathiri kuta za njia ya uzazi. Wasichana wa chini ya umri wa miaka 18 ndio wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo. Ingawa hivyo, wanawake waliokomaa pia wanaweza wakapata ugonjwa huo,” anaeleza Dkt Kimani.

  • Tags

You can share this post!

Ni upumbavu kunizuia kuzungumzia watu wangu Turkana, Raila...

Watu wanne wakiwemo watoto wawili waaga dunia kwenye ajali...

T L