• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
MWANAMUME KAMILI: Maisha mazuri ni gharama, hamna vya dezo na bwerere

MWANAMUME KAMILI: Maisha mazuri ni gharama, hamna vya dezo na bwerere

Na DKT CHARLES OBENE

USIMAMIZI mbovu haujaanza vyuoni.

Asili ya usimamizi duni umechipuka nyumbani na kwenye ofisi za umma serikalini.

Gadhabu za watoto zinapasa kuelekezwa kwa baba na mama zao nyumbani wala sio kwa walimu na mali ya umma vyuoni.

Wanaotaka maisha ya kifalme na umalikia hawana budi kufidia gharama ya maisha ya juu! Maisha mema ni gharama.

Hakuna vya dezo na bwerere!

Maisha mema ni pesa nazo pesa zinaletwa kutoka mifuko ya baba na mama waliowatuma vyuoni.

Kama lazima kuchoma mali, watumwe nyumbani mahambe hawa wakachome vitanda vya jamvi vyumbani na vikombe vya plastiki nyumbani kwao.

Haiwezekani kulipa vichele vya pesa kama karo ya elimu kisha watoto wakaanza kulilia mayai, nyama, kuku na vibanzi vyuoni.

Ukweli ni kwamba vyuo vya humu nchini vinadai na vinadaiwa pesa hata huduma za kimsingi muhali kuviona. Kisa na maana? Wazazi hawalipi karo nayo hazina ya Serikali Kuu imekwisha kauka mfano wa mito ya jangwani!

Tufanyeje nyie mnaotaka lishe na maisha bora vyuoni? Tuwapike walimu na wafanyakazi vyuoni? Zindukeni nyie mnaolalama na kuwalaumu walimu.

Wenye pesa walikwisha kuwapeleka watoto wakasome ughaibuni. Wengine wanalipa pesa za heshima kwenye vyuo vya walalahai!

Akina sisi tunaosoma kwa hiari ya umma na msaada wa serikali ndio kwanza tunachoma mabweni ya vyuo!

Sio jambo geni hasa hapa nchini kwetu kusikia na kuona mabweni ya vyuo yakiteketea katika sehemu mbalimbali.

Wanagenzi wamefanya mazoea “kueleza gadhabu zao” kupitia kuteketeza mali ya umma vyuoni.

Sijui lini mtu mwenye akili timamu na mawazo chanya anaweza kuzua hasara kama njia ya “kujieleza!”

Watoto hawa wanaochoma mali ya umma na wazazi wao wanahitaji tiba kwa dharura kuwaponya magonjwa hayo ya akili. Hawa ni wagonjwa!

Tuacheni kuharibu pesa za umma kulipia karo watoto wasiotaka kusoma.

Na kama lazima kuwalipia na sheria zifuatwe kuhakikisha kuwa wanaopokea pesa za umma wanawajibika ipasavyo.

Lau kuharibiwa vyuoni, hizo pesa za umma zingalifaa watu wa maeneo kame angalau kuwachimbia visima vya maji kwa manufaa ya nyumba na mifugo wao.

Wangalikuwa wanalipiwa karo shuleni na baba na mama zao, watoto hawa wangaliwajibikia masomo ipasavyo.

Tangu lini ukaona vyuo vya walalahai vikiteketezwa na wanafunzi majahili?

Mfumo wa “elimu ya bure” umetufanya kuhuisha “akili za bure”.

Eti watoto wanagadhabishwa na usimamizi vyuoni! Wanatoka wapi watoto hawa wanaotaka kupakatwa shuleni?

Si hawa watoto wanaolelewa na wajakazi na mwinyi nyumbani kwao? Si hawa watoto waliotelekezwa na baba na mama zao wakaachwa kuerevukia vichekesho vya vibonzo?

Kwa nini hawajachoma nyumba ama kuharibu mali yao nyumbani?

Vyuo vinadai malimbikizi ya karo ya wanafunzi kutoka Serikali Kuu hali kadhalika wazazi wa watoto hawa. Vyuo havina pesa kwa kuwa wazazi na serikali hawana pesa!

Walimu wakuu hawawezi kugeuka vitoweo kwa manufaa ya watoto wanaotaka lishe bora.

Isitoshe, baba na mama ya watoto hawa wanashinda mahakamani kuteta juu ya ongezeko la gharama ya elimu.

Wanataka karo ipunguzwe zaidi lakini vyuo viboreshe chakula na makazi ya watoto wao. Hizo ndizo akili za karne ya utandawazi? Hizo ndizo akili mnazopata kwenye mitandao ya kijamii?

Kuta za shule haziwezi katu kugeuka chakula kwa manufaa ya watoto wanoataka lishe bora.

Vyuo na wasimamizi vyuoni wanahitaji pesa tena kwa dharura ili kuboresha hali na maisha shuleni. Huo ndio ukweli unaopasa kukita akilini mwa watoto wanaoteketeza vyuo.

Wajibikeni nyie mnaolaumu hali duni vyuoni kwa kulipa karo inayostahili. Haiwezekani wazazi wanaoshinda mitandaoni kupakua na kupakia sura na midomo yao kuteta juu ya hali duni ya elimu vyuoni.

Usimamizi mbovu umeanza nyumbani kwa watoto hawa wanaochoma mabweni.Watu wazima wanazidi kuwapotosha watoto kwamba ni haki yao kama watoto kulala na kuamka kwa wakati wao!

Eti ni haki kwa mtoto kuchagua mwenyewe anavyopenda kutii na kuzifuata sheria. Sawa.

Lakini afanye hivyo akiwa nyumbani kwao, katika ua la baba na mamake. La ajabu ni kwamba watu wazima hawajajitokeza wazi kusitisha ujahili wanaodhihiri watoto hawa.

Isitoshe, ndio kwanza wanawake kwa wanaume hawa wamepata ufa kukoka moto zaidi kwa kuelekeza lawama katika usimamizi mbovu shuleni.

Lawama wanazobeba walimu na wakurugenzi vyuoni ni njia hasi tu wanazotumia wazazi kukwepa wajibu wa malezi sisemi gharama za kufidia uharibifu vyuoni.

Asili ya uozo huu ni nyumba na vyumba vya wazazi matapeli wanaotaka elimu na maisha ya dezo!

Wenye pesa wanasomea ughaibuni na kwenye vyuo vya walalahai! Hebu tujikune kwa uwezo wetu! Huo ndio ukweli wa mwanamume kamili!

[email protected]

You can share this post!

UMBEA: Kama kweli mnapendana, hakuna kosa lisilosameheka

Manchester City wazamisha chombo cha Manchester United...

T L