• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Waraibu wa asali wanavyouziwa mchanganyiko wa sukari na mwarubaine na wahuni mitandaoni

Waraibu wa asali wanavyouziwa mchanganyiko wa sukari na mwarubaine na wahuni mitandaoni

NA RICHARD MAOSI

WAUZAJI asali kutoka Kajiado na Kitengela wanalalamikia soko la asali kuharibika, kutokana na wafanyabiashara wahuni wanaochakachua bidhaa hiyo muhimu na kuwauzia.

Kulingana na wauzaji hao, mtandao huo wa matapeli unauza dawa chungu ya mwarubaine badala ya asali halisi.

Baadhi yao wanatumia mitandao ya kijamii kunasa wateja ambao hupendelea kununua bidhaa zao kutoka X (Twitter) au Facebook, bila kujua wamepakiwa mkorogo duni kwa kisingizio kuwa ni asali nambari moja.

Kwanza, wanaweka maandishi ya kuridhisha kwenye vipakio na kuambatanisha maelezo maridadi kuhusu manufaa ya kutumia asali, bei ya asali na hapo chini nambari za simu, endapo ungetaka kuwafikia.

Millicent Obonyo mkazi wa Athi River, anasema 2022 aliwahi kuuziwa dawa ya mwarubaine akidhani ni asali kutoka Kajiado.

Alitaka kununua lita tano ya asali mbichi, kwa Sh2,000 ambapo kwake aliona ni bei nafuu ikizingatiwa amekuwa akitumia Sh3,500

Alikutana na muuzaji asali Facebook na akamtumia Sh2, 000, akaahidiwa kwamba angepokea mzigo wake baada ya kufanya malipo.

Waliahidi kumtumia hadi nyumbani kwake lakini alipofungua mzigo wake alishangaa kugundua ameuziwa mchanganyiko wa matope na dawa ya mwarubaine.

“Nilipigwa na uvundo mkali ambao niligundua sio asali kamili na nilipojaribu kuwapigia simu wauzaji, ziliitika tu wala hazikuwa zikichukuliwa na baada ya siku tatu simu zilienda mteja ndiposa nikagundua nilikuwa nimetapeliwa,” akasema.

Kulingana na Obonyo, baadhi ya wauzaji wanatoa ahadi ya kuwapelekea wateja asali mpaka nyumbani kwao ili waweze kuaminika kwa urahisi.

Taifa Leo Dijitali imechakura kumbi za wauzaji wa asali ambao wanakisiwa kuhangaisha wanunuzi.

Kwanza, utagundua kwamba hawana idadi kubwa ya marafiki mtandaoni na pale wanapopata marafiki wachache huanza kubandika bidhaa zao kwa lengo la kutafuta wanunuzi.

Hawana eneo maalum la kuendesha biashara zao na unapotaka kuwatembelea wataanza kukuzungusha.

Obonyo anawashauri wanunuzi kufanya utafiti kuhusu bei ya asali inayopatikana sokoni, badala ya kwenda mtandaoni kusaka wauzaji.

  • Tags

You can share this post!

Pasta Ng’ang’a asema hawezi kupitisha gari lake la...

Pasta Ezekiel ni mweupe kama pamba, Kamati ya Seneti sasa...

T L