• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
PAUKWA: Msanii afumaniwa na Kaburu pabaya

PAUKWA: Msanii afumaniwa na Kaburu pabaya

NA ENOCK NYARIKI

ASUBUHI, Bwana Kaburu aliitembelea Idara ya Parachuti.

Kama ilivyokuwa ada, shughuli zilikuwa nyingi huko kuliko kwingineko mbugani. Parachuti zilikwenda juu kwa umahiri mkubwa.

Katika kila parachuti aliketi mtalii mmoja na mwelekezi wake ambaye angemwonyesha mtalii mahali salama ambapo wangetua.

Watalii wengine walijilaza kwenye viti vya hinzirani idarani hapo huku wakiendelea kuota jua la asubuhi ambalo liliandamana na upepo mwanana.

Walisubiri zamu zao za kuruka angani kwa kutumia parachuti ziwadie.

Kwenye kochi moja lililosimamishwa nje ya jengo moja lenye vyumba vya kubadilisha mavazi, Msanii aliketi huku akiendelea kutafuna udoho ulioachwa na mmoja wa watalii aliyekuwa katika ziara ya kuruka kwa parachuti.

Bwana Kaburu aliyezungukazunguka idarani aliridhishwa na jinsi wafanyakazi wake walivyowashughulikia wageni. Furaha yake ingeendelea kujidhihirisha usoni pake kama asingemwona mwanamume fulani akibwakia mabaki yaliyoachwa na wageni.

Msanii alipofumaniwa na mkubwa wake, alishtuka ghaya ya kushtuka. Aligeuza uso wake ghafla na kutazama upande mwingine.

Aliipinda midomo yake kuelekea upande wa kulia huku akitafuna udoho alioujaza kinywani kwa shida kama aliyekuwa na ulemavu fulani midomoni. Kitendo kile kiliubadili wajihi wake.

Bwana Kaburu alipozunguka ili kumtazama vizuri, Msanii alisimama ghafla akaanza kutembea kwa kuchechemea.
Bwana Karubu hakunena jambo lolote ila alimtazama mpaka alipotokomea nyuma ya majengo.

Aliondoka moja kwa moja kuelekea ofisini alipopiga simu kwa mkuu wa Idara ya Parachuti. Alimuamuru afike ofisini pake mara moja.

HADITHI ITAENDELEA

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Njuguna ni mwalimu mwenye kiu ya utafiti

Atletico yakung’uta Real Valladolid katika La Liga na...

T L