• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
MWALIMU WA WIKI: Njuguna ni mwalimu mwenye kiu ya utafiti

MWALIMU WA WIKI: Njuguna ni mwalimu mwenye kiu ya utafiti

NA CHRIS ADUNGO

MWALIMU anayejali maslahi ya wanafunzi anastahili kujiandaa ipasavyo kwa ajili ya somo lake.

Ajitahidi kuhudhuria vipindi vyote na asome kutoka kwa vyanzo mbalimbali ili awe chemchemi ya maarifa kwa wanafunzi wanaomtegemea.

Kwa mujibu wa Bw Peter Njoroge Njuguna anayefundisha katika shule ya Kahuho Uhuru, Kaunti ya Kiambu, wanafunzi humwamini sana mwalimu aliye na ufahamu mpana wa masomo anayofundisha.

Hivyo, mwalimu bora anastahili kufanya utafiti wa kina katika somo lake na kuchangamkia masuala yote yanayofungamana na mtaala.

“Awahimize wanafunzi mara kwa mara katika safari yao ya elimu, atambue changamoto wanazopitia, aelewe udhaifu na kiwango cha mahitaji ya kila mmoja wao na awaamshie hamu ya kuchapukia masomo,” anasema.

Njuguna alilelewa katika kijiji cha Rurii, Kaunti ya Nyandarua. Ndiye kitinda mimba katika familia ya watoto watano wa Bw John Kimani na Bi Hellen Wambui.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Dayspring Academy, Nyandarua (1995–2003) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Leshau Boys, Nyandarua (2004–2007).

Ingawa matamanio yake yalikuwa kuwa mtaalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano, alihiari kusomea ualimu (Kiswahili/Jiografia) katika Chuo Kikuu cha Nairobi (2010–2014).

Uamuzi huo wa kujibwaga katika ulingo wa ualimu ulichochewa zaidi na Bw Musa Mirobi na Bi Gichuki waliompokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya msingi na upili mtawalia.

Kabla ya kufuzu chuoni, Njuguna alishiriki mafunzo ya nyanjani katika shule ya Ngobit Boys, Kaunti ya Laikipia. Nafasi hiyo ilimpa jukwaa mwafaka la kuzima kiu ya ualimu na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Aliwahi pia kufundisha katika shule ya Graceland Girls, Laikipia (2014) kabla ya kuhamia Ngobit Girls, Laikipia (2015-2017).

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri mnamo 2017 na kumtuma kufundisha katika shule ya Kahuho Uhuru, Kaunti ya Kiambu.

Mbali na ualimu, Njuguna pia ni kocha stadi wa handiboli, mshairi shupavu na mwanafasihi chipukizi. Aliwahi kushirikisha wanafunzi wake katika mashindano ya Daraja 1203J kwenye tamasha za kitaifa za muziki (KMF) mnamo 2015.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kujiendeleza kitaaluma na kuweka hai ndoto ya kuwa mtaalamu wa masuala ya usoroveya.

Anapania pia kuzamia kikamilifu katika uandishi wa fasihi ili kuendeleza kipaji cha utunzi wa mashairi kilichoanza kujikuza ndani yake mnamo 2013.

Kwa mtazamo wake, kufaulu kwa shughuli nyingi za darasani hutegemea ujuzi wa mwalimu, uelewa wake wa stadi za mawasiliano na wepesi wake wa kubuni mbinu mbalimbali za ufundishaji.

Uzoefu wa Njuguna katika utahini wa Kiswahili na Jiografia umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kushauri, kuelekeza na kuhamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

Kwa pamoja na mkewe Bi Annette Bochere, wamejaliwa mtoto – Phineas.

Bi Annette ni mwalimu wa Kiswahili na Historia katika shule ya Kahuho Uhuru, Kiambu.

  • Tags

You can share this post!

Nakuru City Queens wanyorosha Ulinzi Starlets, Zetech...

PAUKWA: Msanii afumaniwa na Kaburu pabaya

T L