• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
PAUKWA: Uchungu wa mwana aujuaye mama mzazi

PAUKWA: Uchungu wa mwana aujuaye mama mzazi

NA ENOCK NYARIKI

MANENO ya mtoto aliyemjia juu Bi Cheusi asubuhi ile yaliufanya moyo wake kumwenda mbiombio akajikuta akiuliza kwa wasiwasi, “Ni nini! Tulia unieleze vizuri.”

Mtoto hakutamka neno jingine zaidi. Kwa mkono wa kulia, alimwashiria Bi Cheusi amfuate. Bi Cheusi alirusha chini karatasi ya sandarusi yenye dagaa na kumwacha mteja wake akitaharuki.

Mtoto mbele, Bi Cheusi nyuma. Moyo ulimpapa mwanamke yule kwa kufuata mapigo ya hatua za nyayo zake.

Walipofika katika mtaa wa kwanza wa Kisera, mambo yalikuwa yamekwenda kasi mno. Ndimi za moto zilikuwa zimeramba vibanda vingi vya mtaa na kuacha vijinga na majivu nyuma. Majivu ambayo yangeendelea kuwakumbusha wakazi kuhusu mkasa uliotokea wakati ambapo gharama ya maisha ilikuwa imepanda kupindukia. Wakazi hao walilia na kuomboleza huku wamevishika vichwa vyao kwa mshangao.

Tayari ndimi za moto zilikuwa zimeanza kuyatafuna mabati yenye kutu yaliyotumiwa kukijenga kibanda cha mbavu za mbwa cha Bi Cheusi. Ziliyafakamia kwa uchu na tamaa. Saa tatu zilikuwa zimepita ilhali hapakuwapo na isimu ya zimamoto.

Wakazi na wahisani wengine waliofika kuwasaidia kuzima moto walikuwa wamekata tamaa. Kadiri walivyojibidiisha kumwaga maji ndivyo juhudi zao zilivyoendelea kwenda mrisi. Moto uliwakejeli. Ndimi za moto ziliwacheza shere.

Kilio cha mwana wa Bi Cheusi aliyekuwa amepaliwa na moshi wa moto kilimkata mwanamke yule ini. Hawakusema wazee wenye hekima kwamba uchungu wa mwana aujuaye ni mama?

“Lazima utende jambo!,’’ nafsi ya ndani ilimrai Cheusi.

HADITHI ITAENDELEA

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mjadala wa urais una faida kwa wawaniaji na si...

MAPISHI KIKWETU: Sweet and sour chicken

T L