• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 4:07 PM
TAHARIRI: Mjadala wa urais una faida kwa wawaniaji na si busara kuuhepa

TAHARIRI: Mjadala wa urais una faida kwa wawaniaji na si busara kuuhepa

NA MHARIRI

KESHO Jumanne, Wakenya watapata fursa ya kuwaweka kwenye mizani wanaotaka kuwa manaibu wa rais Agosti 9.

Justina Wambui Wamae (Roots Party), Rigathi Gachagua (UDA), Ruth Mucheru Mutua (Agano Party) na Martha Wangari Karua (Azimio) wanatarajiwa kumenyana katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Katoliki (CUEA), Nairobi.

Mjadala wao utatoa mwelekeo na kuwapa fursa Wakenya kufahamu kwa kina yale wanayotarajiwa kutoka kwa watakaoingia ikulu.

Mijadala ya urais ni jambo ambalo limekuwa likiendelea katika mataifa yaliyoendelea kama Marekani. Hapa Kenya, mwaka 2017 vyombo vya habari viliamua kuwe na mjadala kama huo, ili watu wachague rais wakiwa wamesikiza wawaniaji wote wakieleza sera zao. Ni fursa nzuri kwa wawaniaji kufafanua tashwishi zozote au masuala ambayo huenda hayajaeleweka kwenye mikutano ya kampeni.

Mwaniaji urais wa UDA, Dkt William Ruto amewahi kunukuliwa akisema huenda akasusia mjadala huo. Kwamba yeye na mgombea mwenza hawana haja ya kushiriki kwenye mjadala ambapo tayari vyombo vya habari vimechukua msimamo kuhusu anayetakiwa.

Madai haya si ya kweli. Vyombo vya habari si gazeti moja, kituo kimoja cha redio au televisheni. Ni mkusanyiko wa vituo mbalimbali. Walioteuliwa kuendesha mahojiano hayo pia wanatoka vituo mbalimbali, na kubwa zaidi ni kuwa, wanahabari huongozwa na kanuni za taaluma hiyo, na wala si kuuliza maswali kwa niaba ya waajiri wao.

Wasimamizi wa mjadala wa urais waliomba umma utume maswali kwa wote watakaoshiriki mahojiano. Ni maswali hayo yatakayotumika. Haijalishi maswali hayo yatakuwa ya aina gani, muhimu ni kwamba wanaotaka urais na manaibu wao watapata nafasi ya kumaliza uvumi au kueleza ukweli ambao huenda watu hawaufahamu isipokuwa porojo na propaganda zinazoendelezwa mitandaoni.

Ni kweli kuwa huenda Kenya haijafikia kiwango cha Marekani au mataifa mengine ya dunia ambako wananchi hufanya uamuzi uchaguzini kutokana na mijadala ya urais. Lakini pia ni kweli kwamba sasa watu wanaelekea upande huo. Mwanasiasa anapotoa tamko kuhusu sera fulani, wananchi huichambua na kuuliza maswali.

Kura za maoni wiki jana zilionyesha kuna zaidi ya asilimia 15 ya wapigakura ambao hawajaamua watakayempa. Kuna uwezekano mkubwa kwamba, baada ya mjadala wa manaibu hapo kesho na ule wa urais Jumanne wiki ijayo, watu hao watafanya uamuzi wa mwisho.

Dkt Ruto na Bw Gachagua wamekuwa wakiwekwa katika asilimia 37 hadi 39. Asilimia hiyo 15 ya wapiga kura ni muhimu kwao, sawa na ilivyo kwa wagombea wengine.

You can share this post!

Nassir atoa ahadi ya kufuta kodi za kanisa kwa kaunti

PAUKWA: Uchungu wa mwana aujuaye mama mzazi

T L