• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
PAUKWA: Ule mabaki ya watalii Kaburu ajue utakiona!

PAUKWA: Ule mabaki ya watalii Kaburu ajue utakiona!

ENOCK NYARIKI

FOLENI ya watalii iliendelea kuongezeka kwenye sehemu ya mapokezi ya mbuga ya wanyama ya Maasai Mara.

Kwingineko mbugani, shughuli zilienea moto mmoja. Shughuli za wapishi stadi walioandaa mapochopocho anuwai kwa ajili ya wageni.

Shughuli za wafanyakazi wa Idara ya Upangaji waliopita na kupituka vyumba ili kuwaonyesha wageni hao mahali ambamo wangezilaza mbavu zao usiku kucha ama kwa siku na miezi. Tena ujumuishe nyakanyaka ya watalii na waelekezi wao waliozunguka kwa magari ya watalii mbugani. Jinsi mandhari hayo yalivyopendeza!

Kwenye Idara ya Parachuti, hali haikuwa tofauti – shughuli zilikuwa vururu mfano wa moto kwenye kichaka kikavu.

Parachuti zilikwenda arijojo na kuwafanya watalii kufurahia kuyaona mandhari ya kupendeza mbugani kutoka angani. Hata hivyo,mambo yote mbugani yasingeenda jinsi yalivyoratibiwa bila ushauri mwema na uongozi thabiti wa Bwana Kaburu.

Bwana Kaburu alikuwa mzungu aliyeshikilia wadhifa wa umeneja ukurugenzi mbugani. Wafanyakazi wote walimheshimu na pia kumwogopa.

Kwenye Idara ya Parachuti, Bwana Kaburu aliogopwa mfano wa maradhi ya kuambukizwa. Jambo moja lililosababisha woga huo ni msimamo wa Bwana Kaburu kuhusu tabia ya baadhi ya wafanyakazi kula mabaki ya vyakula vilivyoachwa na watalii.

Aliyefumaniwa akila mabaki hayo, alipigwa kalamu baada ya kuumbuliwa na Bwana Kaburu kwa maneno yafuatayo:

“Wewe unadhani unaonesha picha gani unapokula mabaki yaliyoachwa na wageni? Una tofauti gani na kelbu mdoeaji?’’

HADITHI ITAENDELEA

  • Tags

You can share this post!

TALANTA YANGU: Keycee ndiye Messi wa kesho

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu anafaa kuteka saikolojia ya...

T L