• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
MWALIMU WA WIKI: Mwalimu anafaa kuteka saikolojia ya wanafunzi

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu anafaa kuteka saikolojia ya wanafunzi

KUFUNDISHA wanafunzi wa shule za msingi kunahitaji mwalimu kutumia mbinu mbalimbali zitakazompa majukwaa maridhawa ya kushirikiana na watoto kutalii mazingira anuwai ambayo yatachangia kukuza viwango vyao vya ubunifu na kuwaamshia ari ya kuthamini utangamano.

Kwa mujibu wa mwalimu Margaret Musyawa Mutiso wa Kings International Academy jijini Nairobi, uchangamfu na ucheshi wa mwalimu huchochea wanafunzi kumakinikia wanachofundishwa.

“Zaidi ya kuwa na ujuzi wa kufundisha na kipaji cha kutumia vifaa mbalimbali vya ufundishaji, mwalimu bora anastahili kuteka saikolojia ya wanafunzi wake kwa wepesi,” anatanguliza.

“Shughuli za ujifunzaji na ufundishaji zitakuwa rahisi iwapo mwalimu atasikiliza wanafunzi, kuelewa changamoto zinazowakibili na kuwaelekeza ipasavyo hatua kwa hatua.”

“Mwalimu pia ana wajibu wa kutambua na kupalilia vipaji vya wanafunzi wake huku akiwatia moyo wale wanaotatizika kuelewa somo lake. Uhusiano wa karibu kati ya mzazi na mwalimu pia utafunua mengi kuhusu uwezo wa mwanafunzi katika nyanja mbalimbali. Hivyo, ipo haja kwa mzazi kufuatilia kwa makini masomo ya mtoto shuleni,” anashauri.

Margaret alilelewa katika eneo la Mwala, Kaunti ya Machakos. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watatu wa Bw David Mutiso na Bi Patricia David.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Kikaso, Machakos (1995-2002) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Vyulya Girls, Machakos (2003-2006) kisha Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Narok (2008-2011).

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa Margaret msukumo wa kusomea diploma nyingine ya ualimu katika Chuo cha Fortune Educational Centre, Machakos (2014-2017).

Japo matamanio yake yalikuwa kusomea taaluma ya udaktari, aliyemchochea kujitosa katika ulingo wa ualimu ni Bw Lawrence Kyenyeka ambaye alimpokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya msingi ya Kikaso.

Baada ya kuhitimu ualimu, Margaret alianza kufundisha katika shule ya msingi ya Lema, Machakos mnamo 2012.

Alihudumu huko kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuhamia Katumani Junior Academy, Machakos alikofundisha kati ya 2014 na 2015.

Alihamia baadaye jijini Nairobi na akapata fursa ya kufundisha katika shule ya msingi ya Carlin, Donholm (2016-2018) kisha Infill Academy, Komarock (2018-2019).

Margaret amekuwa mwalimu wa Kiswahili na somo la Dini katika shule ya Kings International Academy katika eneo Embakasi tangu Januari 2020.

Mwalimu huyu ambaye pia ni mwandishi stadi wa vitabu vya hadithi anayejivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali za maendeleo ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Isitoshe, anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala walimu wengi ambao hutangamana naye katika makongamano ya kielimu.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Margaret ni kujiendeleza kitaaluma na kuwa mhadhiri wa Kiswahili katika chuo kikuu. Kwa pamoja na mumewe, Bw Anthony Muteta, wamejaliwa mtoto wa kike – Mitchelle Mutheu.

  • Tags

You can share this post!

PAUKWA: Ule mabaki ya watalii Kaburu ajue utakiona!

Salat aingia Kenya Kwanza rasmi

T L