• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
PENZI LA KIJANJA: Asiyekufaa kwa dhiki, ni tapeli wa mapenzi

PENZI LA KIJANJA: Asiyekufaa kwa dhiki, ni tapeli wa mapenzi

NA BENSON MATHEKA

“KWANI nilikufanyia nini ukanichukia hivi?” Peter alimuuliza Alice kwenye arafa.

Alice hakujibu ujumbe huo. Hakuona sababu ya kuujibu kwa sababu Peter alimuacha alipokuwa akimhitaji zaidi.

Mwanadada huyu alikuwa amelazwa hospitali baada ya kuhusika kwenye ajali siku chache baada ya kupoteza kazi yake. “Peter hakuwa na mapenzi kwangu. Alikuwa akinitumia tu wakati mambo yangu yalikuwa mazuri na nilipopata matatizo akaniacha,” asema Alice ambaye alipona na kupata kazi nzuri zaidi.

Watalaamu wa masuala ya mahusiano wanasema kwamba watu wenye hulka kama za Peter wamekuwa wakifanya wengi kusononeka.

“Ni matapeli wanaotumia mapenzi kuwanasa wasio na habari. Wakati una afya na pesa wanaganda kwako na kukupagawisha kwa maneno matamu kwa kuwa wanafaidika na jasho au mwili wako. Ukipata shida, wanatoweka. Unaweza kujua mtu anakupenda kwa dhati akisimama na wewe kwa kila hali,” asema mtaalamu wa mapenzi Daisy Muthoni wa Shirika la Abudant Love jijini Nairobi.

“Akikwama kwako unapopitia hali gumu na pia mambo yakiwa sawa, baini ana mapenzi ya dhati kwako, kwama kwake pia. Hii ni moja ya ishara ya wazi ya kujua jinsi mtu anavyohisi wakati unapopitia kipindi kigumu maishani. Iwapo mtu hawezi kukusaidia wakati wa shida ndogo, hakuna uhakika kwamba unaweza kumtegemea ukipatwa na dhiki kubwa,” asema Muthoni.

Mtaalamu huyo anasema mtu aliye tayari kwa uhusiano wa kudumu huwa anafungua moyo wake kwa mpenzi wake. Kauli anayokubaliana nayo Samuel Kimanthi, mwanasaikojia katika kituo cha Big Hearts jijini Nairobi.

“Mtu anayekujali, anakusikiliza nawe unamsikiliza na kumjali sio kwa maneno mbali pia kwa vitendo. Mawasiliano ndiyo hudumisha mapenzi hivyo uhusiano hauwezekani wahusika wasipowasiliana,” asema na kuongeza kuwa kusemezana ni tofauti na kuwasiliana.

Muthoni asema mawasiliano huwa yanawezesha vitendo na kauli za kudhihirisha mapenzi.

“Pasipo na mawasiliano kuna kununa au kulaumiana na ugomvi. Palipo na mawasiliano pana kauli za dhati za kushehenezana sifa, kufarijiana na kudekezana bila kujali hali inayomkabili mmoja wa wahusika. Shida ya mmoja huwa ni shida ya wahusika wawili,” asema Muthoni.

Katika hali hii, aongeza Kimanthi, wachumba huwa wanasaidiana kukua.

“Inaweza kuwa ustawi wa kikazi, kuongeza masomo au kulipa kodi ya nyumba. Pia mnatenga wakati wa kuwa pamoja kulishana mapenzi licha ya shughuli na mahangaiko ya kimaisha,” asema.

You can share this post!

Bodaboda sasa wapumua msako ukisimamishwa

Majeshi ya Putin sasa yabisha Kyiv

T L