• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Majeshi ya Putin sasa yabisha Kyiv

Majeshi ya Putin sasa yabisha Kyiv

NA AFP

KYIV, UKRAINE

VIKOSI vya Urusi jana Jumamosi vilirikaribia jiji kuu la Ukraine, Kyiv, huku mashambulio yake yakiyalenga makazi ya raia katika miji mingine nchini humo.

Jana Jumamosi, Amerika na Umoja wa Ulaya (EU) zilitangaza kuongeza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi.

Mashambulio hayo yaliibua hofu kuwa huenda yakasababisha “mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu” kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni.

Tayari, Umoja wa Mataifa (UN) umesema Urusi inatekeleza uhalifu wa kibinadamu hasa katika jiji la Mariupol, ambapo vikosi vyake vimekuwa vikiuzingira kwa siku kadhaa.

Ijumaa, maafisa wa serikali katika jiji hilo walisema kuwa zaidi ya watu 1,500 wameuawa kwenye mapigano hayo ambayo yamedumu kwa siku 14.

Manusura wamekuwa wakijaribu kutorokea makombora yanayorushwa na Urusi katika jiji hilo bila mafanikio yoyote.

Kando na mashambulio hayo, jiji hilo limeachwa bila maji na chakula.

“Hali katika jiji hili ni ya kusikitisha,” akasema mfanyakazi mmoja wa Shirika la Madaktari Wasio Mipaka.

“Mamia ya maelfu ya watu wamezingirwa,” akasema Stephen Cornish, aliye mmoja wa wale wanaoongoza shughuli za utoaji misaada za shirika hilo nchini Ukraine.

“Kuwazingira watu wanaohitaji misaada si mbinu inayokubaliwa na sheria za kimataifa kuhusu vita,” akaongeza.

Huku Urusi ikiendelea na mashambulio hayo, mazungumzo kati ya taifa hilo na Ukraine yalionekana kutopata mafanikio yoyote.

Rais Volodymr Zelensky sasa analiomba Shirika la Kujihami (NATO) kuingilia kati ili kukabili mashambulio ya Urusi dhidi ya raia wake.

UN ilisema kufikia Jumamosi, watu 2.5 milioni walikuwa tayari washatoroka vita hivyo huku wengine zaidi ya milioni mbili wakiachwa bila makao.

Ijumaa, Rais Joe Biden wa Amerika aliondoa uwezekano wowote wa kuishambulia Urusi moja kwa moja kwa jeshi, akionya kuwa huenda hatua hiyo ikasababisha “Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia.”

Badala yake, alitangaza kuongeza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi.

Alisema Amerika itakata mahusiano yake yote ya kibiashara na Urusi huku akipiga marufuku bidhaa zote kutoka taifa hilo kama vile pombe aina ya Vodka na madini.

Amerika pia ilisimamisha usafirishaji wa bidhaa za mapambo nchini Urusi.

“Lazima (Vladimir) Putin alipe gharama. Hawezi kuanzisha vita ambavyo vinatishia na kutikisha msingi na uthabiti wa amani ya kimataifa na baadaye kuomba msaada kutoka kwa jamii ya kimataifa,” akasema Biden, alipohutubu katika Ikulu ya White House.

Kauli yake ilijiri huku UN ikisema kuwa kufikia jana, watu 2.5 milioni walikuwa tayari washatoroka vita hivyo huku wengine zaidi ya milioni mbili wakiachwa bila makao.

Yulia, 29, ambaye ni mwalimu aliyetoroka Mauripol, alisema mama mkwewe bado amekwama katika jiji hilo, ambapo anasema kuwa mashambulio ya kijeshi bado yanaendelea.

“Kuna miili mingi iliyotapakaa kwenye barabara za jiji hilo ila hakuna yeyote wa kuizika,” akasema.

Kwenye video iliyotolewa jana, Rais Zelensky aliwarai mama wa wanajeshi wa Urusi kutokubali wanao kutumwa kwenye vita hivyo.

“Ningependa kusema haya kwa mara nyingine, nawaomba mama wa wanajeshi wa Urusi kutokubali wanao kutumwa vita katika nchi ya kigeni,” akasema.

Katika jiji la Kharkiv, madaktari katika hospitali moja walirejelea tukio ambapo walitumia siku mbili kutoa jivu kutoka kwa tumbo la mtoto wa miaka minane, ambaye makazi yao yaligongwa na kombora la Urusi.

“Kando na tumbo lake, aliathiriwa vibaya mapafuni,” akasema daktari mmoja anayemtibu mtoto huyo.

Miji ya Kharkiv na Mauripol imebaki kama mahame, hasa katika maeneo ambako vikosi hivyo vinaelekeza makombora yake.

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Asiyekufaa kwa dhiki, ni tapeli wa mapenzi

Ronaldo abeba Man-United dhidi ya Tottenham ligini

T L